Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba wamehimizwa kushiriki kikamilifu kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotazamiwa kufanyika kote nchini ifikapo Novemba 27 mwaka huu.
Hamasa hiyo imetolewa na ndugu Anibariki Ngata, ambaye ni Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Wilaya Mlimba, alipomwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwenye maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Anaye ishi Kijijini, ambayo kwa ngazi ya Halmashauri yalifanyika mwishoni mwa juma lililo pita, tarehe 18.10.2024 kwenye Kitongoji cha Mgudeni, Kijiji cha Luvilikila, Kata ya Mngeta.
Ndugu Ngata aliwahimiza wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi wa Serikali za Mitaa kwa sababu mwananchi ye yote mwenye sifa stahiki za kupigiwa kura, anayo haki ya kugombea nafsi hizo bila kujali Jinsia ama ulemavu.
Nao Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Mlimba, ambao ndio waliokuwa waratibu wa maadhimisho hayo walipata fursa ya kutoa elimu kuhusu Virusi vya UKIMWI (VVU), ulinzi wa mtoto, ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni na elimu ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Washiriki nao walipata fursa ya kuibua changamoto zinazo wakabili katika kijiji chao na baadae wakatoa maoni na mapendekezo ya nini Serikali ifanye kwa kushirikiana na wanakijiji ili kuzitatua.
Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Anayeishi Kijijini hufanyika ili kutambua nafasi ya wanawake wanaoishi vijijini, changamoto zinazo wakabili na kuzitafutia ufumbuzi ili kuweza kupanua wigo wa wanawake wa vijijini kushiriki kikamilifu katika fursa zote za maendeleo zinazopatikana kwenye maeneo yao.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa