Pichani juu: Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero ndugu David Ligazio akiwa katika kikao cha Baraza la madiwani
MADIWANI katika halmashauri ya Wilaya ya Kilombero wamewaagiza wataalamu katika halmashauri hiyo waangalie eneo gani katika Kata tatu patakapofaa kujengwa hospitali ya serikali ya halmashauri hiyo.
Agizo hilo limetolewa Jana katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo ambapo pamoja na mambo mengine pia kulifanyika uchaguzi wa makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
Kata zilizopendekezwa na madiwani hao ili mojawapo paweze kujengwa hospitali hiyo ni Namwawala,Chita au Mngeta.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo David Ligazio alisema madiwani waliridhia ujenzi wa hospitali hiyo kujengwa katikati ya Wilaya ili kuondoa msongamano na umbali wa kutoka eneo moja kwenda eneo jingine.
Diwani wa kata ya Namwawala Muya Msulwa alisema wao wameshatenga maeneo kwa ajili ya ujenzi huo na wananchi wanasubiri kwa hamu ukizingatia kuwa kata hiyo ipo katikati ya Wilaya.
Lakini Diwani wa kata ya Idete Edward Kitaly alisema kuwa ujenzi wa hospitali hiyo Namwawala unaweza ukaikosesha halmashauri hospitali kwani taarifa alizonazo ni kwamba Kata ya Ifakara inaweza kuwa jimbo hivyo kata ya Namwawala kuweza kumezwa na kuingizwa halmashauri ya Mji Ifakara na kushauri hospitali hiyo kusogezwa eneo la Mngeta ama Chita.
Baada ya majadiliano ya muda mrefu, ndipo Mh. Ligazio aliwataarifu wajumbe wa kikao hicho kuwa wataalamu wa halmashauri wanatakiwa kuangalia mapendekezo ya madiwani na kuona wapi kutafaa ujenzi wa hospitali hiyo
Awali ilielezwa kuwa halmashauri inataraji kupata Fedha kiasi cha shilingi milioni 500 toka hazina za kuanza ujenzi wa hospitali ya halmashauri ya Wilaya na fedha hizo zinaweza kuletwa wakati wowote kutoka sasa.
Ligazio alisema mapendekezo yalielekeza hospitali ijengwe eneo la Namwawala kwani pamoja na vigezo vingine vya kisekta,vikao vya serikali za vijiji na Kata katika Kata husika vimeainisha maeneo mawili yenye zaidi ya ekari 30 kila eneo kwa ajili ya mradi huo.
Alisema maeneo yaliyopendekezwa hayakuwa na fidia kwani ni ya serikali na baada ya taarifa hiyo kuwasilishwa kamati iliridhia hospitali ya halmashauri ya Wilaya ijengwe katika jimbo la Mlimba isipokuwa wajumbe wanaotoka eneo la jimbo hilo wakubaliane eneo itakapojengwa hospitali hiyo kulingana na vigezo vilivyowekwa
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa