Katibu tawala mkoa wa Morogoro Mh. Clifford Tandari ameipongeza halmashauri ya wilaya Kilombero kwa kuendesha kwa ufanisi mkubwa zoezi la utambuzi wa mifugo hali inayopelekea Halmashauri zingine kuja kujifunza jinsi Kilombero ilivyoweza kufanikisha zoezi hilo la utambuzi wa mifugo kwa ufanisi.
Mh Clifford tandari ameyasema hayo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya utumishi wa umma ambapo alizungumza na watumishi wa wilaya ya Kilombero katika kikao ambacho kiliwakutanisha kwa pamoja watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero na watumishi wa halmashauri ya mji Ifakara.
Katibu tawala mkoa wa Morogoro ametumia fursa hiyo kuwasisitiza watumishi wa umma kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kwa kuzingatia miongozo ya kazi (Standing Order) pia amewaasa watumishi kuzingatia miongozo ya mavazi wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi na kuwapongeza watumishi wa wilaya ya Kilombero kwa kuzingatia mwongozo wa mavazi kwa vile wanavyoonekana nadhifu kadri mwongozo unavyohitaji.
Awali Mh. Clifford Tandari alipata utambulisho kutoka kwa kila mtumishi ambapo kupitia utambulisho huo aliagiza kwa kila mtumishi ni vyema akavaa vitambulisho vidogo vya serikali ili atambulike rasmi kwa kuzingatia mwongozo wa utengenezaji wa vitambulisho hivyo vya kazi huku akimuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero kuwapatia watumishi wake vitambulisho hivyo katika kipindi cha mwezi mmoja kutoka sasa.
Vilevile katibu tawala amewahimiza watumishi kufika kazini kwa wakati kuanzia saa 1: 30 mpaka saa 9:30 na kuwashauri wakurugenzi watendaji wa Halmashauri ya wilaya Kilombero na Halmashauri ya Mji Ifakara kuwawezesha kwa kuwapatia nauli au usafiri wa pamoja watumishi wanaokaa mbali na maeneo ya kazi ili waweze kufika kazini kwa wakati, pia ameagiza matumizi ya mashine za kumtambua mtumishi anapoingia na kutoka kazini kwa kutumia teknolojia ya biometric.
Katika kuzingatia falsafa ya matokeo amewataka watumishi kuzingatia muda na kuyapata matokeo kwa wakati kulingana na malengo waliyojipangia watumishi na halmashauri kwa pamoja na uboreshaji wake uonekane katika ngazi ya mwananchi, amewataka watendaji kuwa wabunifu katika kuwasaidia wananchi ili kuleta matokeo mazuri.
Akichanganua mahitaji ya kila idara kulingana na changamoto zilizopo Mh. Clifford Tandari amewaagiza kwa pamoja mganga mkuu na afisa maendeleo ya jamii kutatua changamoto ya ugonjwa wa malaria na HIV katika halmashauri ya wilaya ya Kilombero huku akimuomba mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero kutumia vizuri fedha za wafadhili zinazofadhili miradi mbalimbali ya afya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha dispensali na vituo vya afya vinakuwa na dawa wakati wote.
Katibu tawala huyo amewataka viongozi wa elimu kuboresha viwango vya elimu kwa mkoa wa morogoro kwa kuboresha viwango vya ufaulu na kuhakikisha vifaa vya elimu maalum vinafika kwa walengwa kwa wakati na kuhakikisha mapungufu yaliyopo yanarekebishwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha madeni ya walimu yanashughulikiwa mapema kwa kutumia utaratibu wa P4R.
Wakati huohuo Mh. tandari amewahimiza watendaji wa Kilimo, mifugo na uvuvi kuendeleza juhudi wanazozifanya katika kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji huku akiwapongeza kwa mafanikio waliyoyafikia kwa sasa kwa kupunguza migogoro hiyo ya wakulima na wafugaji kwa mafanikio makubwa na amewatahadharisha kuchukua tahadhari kwa kipindi hiki cha sasa ambapo mvua zimeisha hivyo wafugaji wataanza kurudisha mifugo yako kwenye maeneo yao.
Amezitaka idara za ujenzi , maji, fedha pamoja na kitengo cha manunuzi kuachana na dhana ya kujipatia fedha kutoka kwa wakandarasi na badala yake wafanye kazi kwa uaminifu kwa kuzingatia sheria ,kanuni na taratibu huku akiwasisitiza wahandisi kuzingatia viwango vya ujenzi wa barabara na waache kucheza na wakandarasi ili waweze kufanya kazi kwa uadilifu, pia amemtaka mhandisi wa maji kuhakikisha miradi yote ya maji inatekelezwa kwa wakati ili iweze kuwahudumia walengwa.
Kwa kuzingatia utoaji wa huduma bora Mh. Tandari ambaye ndiye mtendaji mkuu wa watumishi wa umma kwa ngazi ya mkoa amewataka watunza kumbukumbu pamoja na wakuu wa idara kutunza siri za ofisi ikiwa ni wajibu wa kila mtumishi kuhakikisha siri za taasisi hazitoki nje kwa njia yoyote ile. Amewaomba madereva kutotangaza yale wanayoyasikia kutoka kwa viongozi wanaowahudumia huku akitumia nafasi hiyo kuwaomba wakurugenzi kuwapatia posho zao madereva mapema wanapokuwa safarini na kuwaomba madereva kuyatunza magari wanayoyatumia na kuyafanyia matengenezo kwa wakati.
Akihitimisha Kikao chake na watumishi wa wilaya ya Kilombero amewataka viongozi wa utamaduni na michezo kuhakikisha wanainua na kukuza vipaji mbalimbali vya wachezaji ikiwa ni pamoja na kuendeleza juhudi za kutoa msaada wa kuzisaidia timu za mpira wa miguu za Shupavu na Mkamba rangers ili ziweze kufanya vizuri na hatimae kuzipandisha daraja.
Akitoa shukrani zake kwa katibu tawala mkoa wa morogoro mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero Mh. Dennis Lazaro londo amemuhakikishia katibu tawala kuwa halmashauri yake itazingatia maelekezo yote aliyoyatoa kwa kubeba dhamana ya kuwakilisha wengi kwa kuzingatia matakwa ya serikali yetu chini ya uongozi wa raisi John Joseph Pombe Magufuli.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa