Halmashauri ya wilaya ya Kilombero imepongezwa kwa kupata hati safi kutoka kwa mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali(CAG)kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt Kebwe Steven Kebwe katika hotuba yake iliyosomwa na ndugu, Ramadhani Kazimoto katibu tawala msaidizi serikali za mitaa morogoro aliyemwakilisha katika kikao cha baraza la madiwani wa halamashauri ya wilaya ya Kilombero kilichofanyika Julai 28,2017.
Katika hotuba hiyo Dkt Kebwe alisema halmashauri ya wilaya ya Kilombero tangu mwaka wa fedha wa 2013/14 hadi mwaka wa fedha wa 2015/16 imekuwa ikipata hati safi inayoridhisha jambo aliloeleza kwamba linastahili pongezi kwakuwa ni halmashauri chache nchini ambazo zimekuwa zikipata hati safi zinazoridhisha kwa mfululizo.
‘Mimi tangu nimefika katika mkoa wa Morogoro ,nimekuwa nikishuhudia kila mwaka mkipata hati safi inayoridhisha hivyo nawapongeza na nawaomba muendeleze hali hii na ikiwezekana mpate hati ya kiwango cha ubora zaidi ili halmashauri hiii iendelee kuwa mfano kwa halmashauri zingine katika mkoa wa Morogoro na nchi kwa ujumla’.
Aidha alitumia fursa hiyo kuishauri halmashauri ya wilaya ya Kilombero kuyafanyia kazi mapendekezo yanayotolewa na ofisi ya makaguzi mkuu wa hesabu za serikali ili iweze kufikia kiwango cha asilimia 20% ya uchangiaji wa bajeti yake ya ndani.
Kwa upande wake mdhibiti na mkaguzi wa serikali mkoa wa Mororogoro ndugu, Mwabwanga alieleza kuwa Katika mwaka wa fedha wa 2015/16 mdhibiti na mkaguzi wa mahesabu ya serikali alifanya ukaguzi katika mamlaka za serikali za mitaa 171 ambapo ilibainika kuwa halmashauri 138 zilipata hati inayoridhisha ambapo kati ya hizo halmashauri tano zilitoka mkoani Morogoro ikiwemo halmahauri ya wilaya Kilombero, jambo aliloeleza kuwa ni la kujivunia.
Bwana Mwabwanga aliongeza kuwa, mkoa wa Morogoro umefanikiwa katika baadhi ya Halmashauri zake kupata hati zinazoridisha ikiwemo halmashauri ya wilaya ya Kilombero ambayo ndiyo iliyoongoza ambapo pia kuanzia mwaka 2011/12 hadi 2015/16 imeendelea kupata hati inayoridhisha na pia imekuwa ikiyafanyia kazi mapendekezo ya mkaguzii mkuu wa mahesabu ya serikali nchini kwani ilikuwa na mapendekezo 52 ya kuyafanyia kazi na mapendekezo 49 kati ya hayo yametekelezwa ikiwa ni sawa na 94% ya utekelezwaji aidha kamati ya kudumu ya hesabu ya serikalii za mitaa ilitoa maagizo 10 kwa halmashauri ya wilaya ya Kilombero mwaka 2013 ambapo maagizo hayo yalitekelezwa kwa asilimia zote na hivyo kuipongeza kwa ufanisi huo.
Aidha aliwaomba madiwani pamoja na watendaji wa serikali kushirikiana ili kuweza kufikia lengo la kukusanya bilioni 3.3 kwa kuhakikisha kwamba mifumo rasmi ya ukusanyaji wa mapato ya serikali inatumika ipasavyo, huku akitumia fursa hiyo kuelezea athari za ucheleweshwaji wa fedha za shughuli za maendeleo katika halmashauri zilizopo mkoani Morogoro.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero ndugu Daudi Ligazio alisema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2016/17, halmashauri ya wilaya ya Kilombero iliazimia kukusanya bilioni 3.6 na kufanikiwa kukusanya asilimia 92 ya fedha hizo na kuongeza kuwa halmashauri imefanikiwa kupeleka fedha katika miradi mbalilmbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya ujenzi wa nyumba za waalimu, vyoo, madawati pamoja na utekelezwaji wa miradi ya maji katika vijiji 14, pamoja na ukarabati wa barabara kwa kwa ufadhili wa jumuiya ya Ulaya(Barabara ya Chita - Merela) na kufafanua kuwa jiografia ya halmashauri ya wilaya hiyo imekuwa ni changamoto kubwa inayopelekea uchelewaji wa kukamilika kwa miradi mingi kwa wakati na kuahidi kuwa wataendelea kuyafanyia kazi mapendekezo ya mkaguzi wa hesabu za serikali.
Kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Julai, 28 mwaka 2017 ni kikao cha mwisho kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 ambapo pia pamoja na mambo mengine baraza hilo lilifanya uchaguzi wa makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo kwa kumchagua Bwana Emmanuel Ndangalasi (CCM), kupitisha muhtasari wa kikao kilichopita na kushiriki katika zoezi la upimaji wa Afya wa hiari huku pia likihudhuriwa na wajumbe wote wa baraza hilo wakiwemo katibu tawala wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero aliyemuwakilisha mkuu wa wilaya hiyo wabunge wa majimbo ya Kilombero na Mlimba , viongozi wa vyama vya siasa, wadau wa maendeleo pamoja na wananchi wakazi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero.
Mwandishi ; Ibrahim Rojala
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa