Katibu Tawala wilayani Kilombero Mh. Robert Selasela ametoa ushauri kwa wazazi kuongeza ushirikiano na walimu ili kuondoa uadui baina ya wazazi na walimu na badala yake wazazi kupitia umoja wa wazazi (UWAWA) wawe sehemu chanya ya kusababisha wanafunzi kujifunza ili kuimarisha elimu ya mtoto shuleni, katika kuhakikisha mwanafunzi anajifunza vyema. katibu tawala amewaomba UWAWA kuwashawishi wazazi wenzao kuchangia ili kuwawezesha wanafunzi kupata mlo wanapokuwa shuleni pia amewataka walimu pamoja na viongozi wa kisiasa katika ajenda zao za vikao kuwashawawishi wazazi umuhimu wa kupata mlo wanapokuwa shuleni ili waweze kupata elimu bora na walimu watapata fursa ya kuwawekea maarifa kwa muda wote wanapokuwa shuleni, Selasela ameyasema hayo katika maazimisho ya Wiki ya Elimu - Kilombero yaliyofanyika Mang'ula kata ya Mwaya.
Awali katibu tawala alitembelea maonesho ya zana za kufundishia na kushuhudia walimu pamoja na wanafunzi wakitumia zana za asili na za kisasa kufundishia ambapo alitumia muda huo kuwasisitiza walimu kwamba zana hizo zisiishie kwenye maonesho tu bali pia ziendelee kutumika darasani ili kuwaandaa vizuri wanafunzi kwa kuwajengea msingi wa elimu kwa vitendo ambapo wanafunzi mara baada ya kuhitimu masomo yao wawe ni watu bora kuitumia elimu yao kwa vitendo.
Aidha Mh. Selasela ameagiza walimu kuendeleza vipaji vya wanafunzi ambao wametengeneza zana za kufundishia ili kukuza vipaji vyao na kuhuisha dhana ya elimu ya kujitegemea ambapo vipaji vyao vitatumika kuwanufaisha katika maisha yao ya baadaye, wakati huohuo katibu tawala Kilombero amewaelekeza wataaluma na walimu wa shule za msingi kuona umuhimu wa kuwafundisha wanafunzi masomo ya sayansi kwa vitendo (practical) ili mwanafunzi anapofika sekondari apate muendelezo wa practical kwa urahisi na ufasaha zaidi.
Akitoa hotuba yake Katibu tawala huyo amemuagiza Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri kwa kushirikiana na afisa elimu sekondari kuwawezesha walimu wanaotumia teknolojia ya sayansi kuwafundisha wanafunzi kwa kuwanunulia vifaa vya teknolojia ya habari na mawasiliano badala ya walimu hao kutumia vifaa vyao binafsi, aliyasema hayo baada ya kushuhudia ufundishaji wa mfumo wa jua linavyozunguka kwenye mhimili wake huku mzunguko huo ukiwa unaonekana kwa kutumia mashine ya projector ambapo vifaa vilivyokuwa vinatumika ni vya wenyewe walimu binafsi.
Bwana Selasela aliendelea kusisitiza kwa kuwaomba wadau wa elimu Kilombero shirika la Plan International kukisaidia kituo cha ufundi Kisawasawa ili taasisi hiyo ya ufundi iwe ni sehemu ya kimbilio la kuwasaidia vijana wa Kilombero katika kujifunza stadi za ufundi, pia amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kilombero kufanya jitihada za makusudi kukitangaza zaidi kituo hicho cha ufundi nje ya Kilombero ili mkoa mzima uweze kukifahamu na kupelekea watu wenye uhitaji wa mafunzo yanayotolewa na kituo waweze kujiunga na chuo hicho cha ufundi Kisawasawa.
Akihitimisha khotuba yake Mh. Selasela amewataka walimu kuendelea kutimiza majukumu yao kwa kutoa maarifa kwa wanafunzi wakati serikali ikiendelea kuwajibika kutatua changamoto zao,huku akiwataka walimu hao kuachana na visngizio vya kila siku pamoja na kuachana na siasa wakati wanapotimiliza majukumu yao shuleni.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa