Wilaya imepakana na Wilaya za Kilosa na Kilolo kwa upande wa Kaskazini Mashariki; na upande wa Kusini imepakana na Wilaya ya Ulanga. Kwa upande wa Mashariki imepakana na Wilaya ya Morogoro Vijijini na Magharibi imepakana na Wilaya za Njombe na Mufindi.
MAENEO YA UTAWALA
Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero ina majimbo mawili ya Uchanguzi ambayo ni Jimbo la Kilombero na Jimbo la Mlimba, tarafa 4 ambazo ni tarafa ya Kidatu, Mang’ula, Mngeta na Mlimba, kata 26, vijiji 99 na vitongoji 398 Wilaya ya Kilombero ina ukubwa wa eneo wa kilomita za mraba 14,532.335. kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Halmashauri ya wilaya Kilombero ina watu 301,456 kwa mwaka 2015.
Hali ya hewa ya Wilaya hii ni ya joto mithili ya pwani kwa wastani wa 26°C – 32°C. Wilaya ina vipindi viwili vya mvua ambavyo ni vuli na masika. Mvua za vuli huanza kunyesha mwezi Novemba na kuishia miezi ya Januari au Februari. Mvua za masika huanza mwezi Machi na kwisha mwezi Mei au Juni. Wastani wa mvua ni kati ya milimita 1,200 hadi 1,600. Kutokana na wingi wa mvua na maeneo mengi kuwa katika bonde la mto Kilombero, mara nyingi hutokea mafuriko katika maeneo mengi ya Wilaya hii.
Sehemu kubwa ya Wilaya ya Kilombero imo katika bonde la Mto Kilombero na kiasi kidogo kiko katika bonde la mto Rufiji na mbuga ya akiba ya wanyama ya Selous. Bonde la mto Kilombero linakingwa na milima ya Udzungwa ambayo pia ni Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa kwa upande wa Kaskazini. Milima hii imefunikwa na kupambwa na miti ya Miombo na pia baadhi ya wanyama ambao ni nadra kuwaona katika Hifadhi zingine za Taifa na hata maeneo mengine duniani. Milima ya Udzungwa ina urefu wa meta 1700 kutoka usawa wa bahari.
Wilaya ya Kilombero ina mito ipatayo 38 ambayo hutiririsha maji yake kwa mwaka mzima. Mito hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa Taifa katika utoaji wa umeme. Vyanzo vya umeme wa Kidatu na Kihansi vimo katika wilaya ya Kilombero. Kwa upande wa kilimo cha umwagiliaji, bado mito hii haijaweza kutumika kikamilifu kwani kwa sehemu kubwa aina ya miradi ya umwagiliaji unaofanyika ni wa kutumia mifereji ya asili na ni kwa sehemu ndogo sana.
HUDUMA ZA KIUCHUMI
Wananchi wengi kadri ya asilimia 80 hujishughulisha na kilimo. Wengi huzalisha, mpunga, mahindi, maharage na migomba. Mazao hayo hutumiwa kwa chakula na biashara pia. Mazao ya biashara ni pamoja na miwa, ufuta na kakao. Mifugo pia ni sehemu ya Uchumi wa Wilaya. Mbali na kilimo shughuli zingine za kiuchumi ni uvuvi katika mto Kilombero na katika mabwawa na mito mingine iliyopo wilayani. Pia kuna makampuni ya uwindaji ambayo hufanya shughuli za uwindaji wa kitalii katika wilaya kando kando ya mto Kilombero na katika eneo la pori la akiba la Selous. Wilaya ya Kilombero ina Mtandao wa barabara zenye urefu wa Km. 868.3 zinazosimamiwa na kuhudumiwa na Mhandisi wa Ujenzi Wilaya pamoja na TANROAD.
IDARA NA VITENGO
1. IDARA YA UTUMISHI NA UTAWALA
Idara ya Utumishi na Utawala ni moja kati ya Idara 13 za Halmashauri (kwa mujibu wa muundo mpya wa Halmashauri) inayosimamia masuala yote ya Utumishi ikiwemo Ajira, Maendeleo ya Watumishi na kutetea haki na maslahi ya watumishi na Mwajiri pamoja na masuala ya kinidhamu kwa Watumishi wote. Idara ya Utumishi na Utawala ndio yenye majukumu ya kusimamia utendaji kazi wa rasilimali watu na utawala kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuwezesha utekelezaji wa malengo ya kazi za Halmashauri ambazo zinatekelezwa kwa kutumia Idara (13), Vitengo (6), Kata 26, Vijiji 99 na Vitongoji 398.
Pia Idara ya Utumishi na Utawala inasimamia ajira za watumishi, kupanda vyeo, kuingiza taarifa mbalimbali za watumishi kwenye mfumo wa Lawson, Ujazaji wa fomu za Upimaji wa wazi wa utendaji wakazi (OPRAS), mafunzo na maslahi ya kikazi kwa ujumla. Baada ya mgawanyo wa watumishi kwa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero na Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Idara ya Utumishi inawatumishi 249 kuanzia ngazi ya wilaya, kata na vijiji.
2. IDARA YA FEDHA NA BIASHARA
Idara ya fedha inawajibu wakutoa ushauri wa masuala ya fedha na taratibu kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo, ukusanyaji wa mapato, kuandaa taarifa za fedha ikiwemo na kujibu hoja za ukaguzi. Idara pia husimamia masuala yote yanayohusiana na biashara na viwanda wilayani. Idara ya fedha katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero ina watumishi 14 wa fedha na biashara 2.
3. IDARA YA MIPANGO, UFUATILIAJI NA TAKWIMU
Idara ya Mipango ni moja kati ya idara za halmashauri ambayo ina jukumu kuu la kuratibu mipango yote ya maendeleo ya wilaya ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wake unazingatia vipaumbele na mgawanyo wa rasilimali kisekta ili kufikia maendeleo endelevu. Aidha Idara inajukumu la kuandaa bajeti na kubuni vyanzo vya mapato. Idara ina watumishi 4 kati yao wachumi ni 2 na Watakwimu ni 2.
4. IDARA YA MIFUGO NA UVUVI.
Idara ya Mifugo na Uvuvi ina wajibu wa kusimamia ufugaji wa mifugo na masuala yote ya uvuvi kwa kuhakikisha shughuli hizo zinakuwa endelevu na zenye tija kwa wafugaji na wavuvi.
Idara hii inao watumishi 21 kati ya watumishi hao Maafisa Mifugo ni 14 na Maafisa Uvuvi 7.
5. IDARA YA KILIMO, UMWAGILIAJI NA USHIRIKA
Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika ina wajibu wa kusimamia shughuli za kilimo na ushirika katika Halmashauri ya wilaya ya kilombero. Idara hii inao watumishi 67 kati ya watumishi hao Maafisa kilimo ni 5, Maafisa kilimo wasaidizi ni 56, Wahandisi wa umwagiliaji ni 2, Afisa Matumizi Bora ya Ardhi ni 1 na Maafisa ushirika ni 3.
6. IDARA YA ELIMU MSINGI
Halmashauri ya wilaya ya kilombero ina shule za msingi 133 kati ya hizo shule za serikali ni 131 na binafsi 2. Pia wilaya ina jumla ya walimu 1,116, Maafisa Elimu 7 na wanafunzi 66,870 kati yao wanafunzi wa shule za awali 7,941 na msingi 58,929. Idara ya elimu msingi inawajibu wa kusimamia utoaji wa elimu katika shule za msingi ili kuboresha elimu na ustawi wa watu. Aidha Idara inajukumu la kusimamia miradi ya elimu inayotekelezwa hapa wilayani kama vile ujenzi wa nyumba za walimu, madarasa, matundu ya vyoo na utengenezaji wa madawati kwa shule za msingi.
7. IDARA YA ELIMU SEKONDARI
Idara ya elimu sekondari inawajibu wa kusimamia utoaji wa elimu katika shule zote za sekondari kwa lengo la kuboresha elimu na ustawi wa watu. Kwa upande wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero idara inaratibu shule 33 za kidato cha nne hadi kidato cha sita kati ya hizo shule 24 ni za kutwa, shule 9 ni za bweni na kutwa. Shule 24 ni za serikali na shule za watu binafsi 9. Idara ina jumla ya walimu 746. Halmashauri ya wilaya ya kilombero ina jumla ya wanafunzi 10,871.
8. IDARA YA UJENZI
Idara ya ujenzi inajukumu la kuhakikisha barabara zote wilayani zinapitika katika kipindi chote cha Mwaka. Idara hii inao watumishi 9 kati ya hao Wahandisi 2, Fundi sanifu 6 na Fundi stadi 1.
9. IDARA YA AFYA
Halmashauri ya wilaya ya Kilombero ina jumla ya vituo 54 vya kutolea huduma za afya , kati ya vituo hivyo 1 ni hospitali ya shirika la Umma, 5 ni vituo vya afya na 48 ni zahanati. Idadi hii inajumuisha vituo 26 ambavyo vinamilikiwa na serikali na vituo 28 vinamilikiwa na mashirika ya kidini na watu binafsi. Kazi kubwa ya Idara hii ni kuhakikisha wakazi wa Halmashauri hii wanapata kinga na tiba kwa maradhi mbalimbali. Idara ina jumla ya watumishi 289.
10.IDARA YA MAJI
Idara ya maji inasimamia utoaji wa huduma ya maji safi na salama mijini na vijijini. Idara hii ya maji huchimba visima vifupi, vya kati na virefu kuhakikisha wakazi wa Halmashauri ya wilaya ya kilombero wanapata maji safi na salama kwa uhakika. Idara ina jumla ya watumishi wapatao 8 kati ya hao Mhandisi 1, Fundi Sanifu 7.
11. IDARA YA ARDHI NA MALIASILI
Idara ya Ardhi na Maliasili ina vitengo vikuu viwili ambavyo ni Ardhi na Maliasili. Kazi kuu ya Idara hii ni kusimamia ugawaji wa ardhi kwa mujibu wa sheria na taratibu, kuhifadhi misitu na wanyamapori kwa maendeleo endelevu. Idadi ya watumishi katika Halmashauri ya wilaya ya Kilombero ni 30 katika ya hao Mthamini 1, Maafisa Mipangomiji 2, Afisa ardhi mteule mmoja 1, Wapima ardhi 4 na Warasimu ramani 2. Kwa upande wa misitu kuna maafisa misitu 11 na Maafisa wanyapori 9.
12. IDARA YA MAENDE LEO YA JAMII
Idara ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii ina wajibu wa kufanya uragibishi, uwezeshaji, uhamasishaji, utetezi, na ushirikishaji jamii katika hatua za kujiletea maendeleo endelevu. Idara ina vitengo vikuu viwili ambavyo ni Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii. Idara inao watumishi 18 wa kitengo cha Maendeleo ya Jamii na watumishi 2 wa kitengo cha ustawi wa jamii. Aidha idara inaratibu shughuli za mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI katika Halmashauri ya wilaya ya Kilombero.
13. IDARA YA USAFI NA MAZINGIRA
Idara hii inalo jukumu la kusimamia masuala yote yanayohusianan na usafi na mazingira katika maeneo ya Halmashauri kwa ujumla. Idara hii inao watumishi 2.
14. KITENGO CHA UCHAGUZI
Kitengo cha Uchaguzi kina jukumu la kusimamia masuala yote yanayohusiana na uchaguzi katika Halmashauri na kutoa ushauri wa jinsi ya kuendesha uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi Mkuu katika Halmashauri. Kitengo hiki kina Mtumishi 1.
15. KITENGO CHA TEHAMA
Kitengo cha TEHAMA kina jukumu la kusimamia masuala yote yanayohusiana na teknolojia, habari na mawasiliano katika Halmashauri na kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya mifumo ya kiteknolojia inayotumika, kusimamia matengenezo ya vifaa vya ofisi na kuhakikisha Halmashauri inakuwa na mahusiano mazuri ya ndani na taasisi za nje. Kitengo hiki kina Mtumishi 1.
16. KITENGO CHA UKAGUZI WA NDANI
Kitengo cha Ukaguzi wa hesabu wa Ndani kina jukumu la kukagua mifumo ya ndani ya kifedha na kutoa ushauri juu ya mwenendo wa ukusanyaji mapato na matumizi unavyofanyika katika Halmashauri. Kitengo hiki ndilo jicho la Halmashauri katika kusimamia rasilimali fedha na watu. Kitengo hiki kina Watumishi 2.
17. KITENGO CHA MANUNUZI
Kitengo cha manunuzi kina jukumu la kuhakikisha manunuzi yote yanayofanyika ikiwa ni pamoja na utunzaji wa vifaa yanafanyika kwa misingi ya sheria na taratibu za manunuzi ya serikali. Kitengo hiki kina watumishi 4.
18. KITENGO CHA SHERIA
Kitengo cha sheria kina jukumu la kusimamia masuala yote ya kisheria kwa kusimamia kesi zote zinazohiusu Halmashauri na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Idara za Halmashauri juu ya masuala ya kisheria. Kitengo hiki kina watumishi 2.
19. KITENGO CHA NYUKI
Kitengo cha Nyuki kina jukumu la kusimamia masuala ya ufugaji wa nyuki kwa kutoa ushauri juu ya ufugaji nyuki wenye tija kwa wafugaji. Aidha kinawaelekeza wafugaji mahala vifaa vinavyotumika katika ufugaji vinapopatikaka na kutoa ushauri wa upatikanaji wa masoko ya asali na nta yanapopatikana. Kitengo hiki kina watumishi 2.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa