Jumla ya wananchi 453 wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba wakiwemo wazee, wajawazito na watoto wamenufaika na huduma za matibabu za madaktari bingwa wa mama Samia waliokuwepo kwenye Hospitali ya Halmashauri hiyo kwa muda wa siku tano kuanzia Juni 3 hadi 7, wakitoa huduma za magonjwa ya ndani, wanawake, watoto, mifupa, upasuaji na ganzi na usingizi.
Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu wa Wilaya Mlimba Daktari Christina Guveti, ambaye pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji wa utoaji wa huduma hizo kwenye Hospitali 184 za Halmashauri mbalimbali kote nchini.
Aidha, Dkt. Guveti amesema yeye pamoja na wasaidizi wake wameona bado kuna uhitaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba, hivyo wanapanga kuweka namna nzuri ya kuhakikisha huduma hizo zitakuwa endelevu Hospitalini hapo.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Halmashauri Dkt. Willy ameishukuru timu ya madaktari bingwa kwa kuzindua huduma za upasuaji hospitalini hapo.
Kwa upande wao wananchi ambao ni miongoni mwa walionufaika wa huduma hizo za kibingwa hospitalini Mlimba wamesema, wameridhishwa na huduma zilizokuwa zikitolewa na madaktari bingwa na wameipongeza Serikali kwa kuona haja ya kuwasogezea wananchi huduma za kinbingwa za matibabu kupitia Hospitali za Halmashauri.
Baadhi yao wamesema ujio wa madaktari hao umekuwa suluhu kwa matatizo ya kiafya waliyodumu nayo kwa miaka mingi bila kujua undani wake.
“Nimesumbuliwa na tatizo la kuvimba miguu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 14 lakini kupitia vipimo nilivyoandikiwa na madaktari hao, tatizo limeweza kugundulika na nimepatiwa dawa ambazo ninaamini zitaponesha kabisa tatizo nililo nalo” alieleza mmoja wa wananchi waliohudhuria hospitalini Mlimba.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba ndugu Jamary Idrisa amewapongeza na kuwashukuru madaktari hao kwa huduma nzuri walizotoa kwa wananchi kwani kupitia hizo wananchi wameweza kuona namna Serikali inavyojali afya za wananchi wake.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa