Jumatatu tarehe 17.11.2025 Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, anayeshughulikia masuala ya afya, Prof. Tumaini Nagu alifanya ziara ya kikazi kwenye Halmashauri ya Wilaya Mlimba kukagua miundombinu na huduma za afya katika Hospitali ya Halmashauri, na Zahanati ya Mbingu.


Kupitia ziara hiyo, Prof. Nagu amesema TAMISEMI itahakikisha inatatua changamoto ya uhaba wa watumishi wa afya hasa katika Hospitali ya Halmashauri, kuleta gari la wagonjwa (ambulance), na kuhakikisha stahiki za watumishi wa afya zinaendelea kulipwa kwa wakati ili kuendelea kuimarisha sekta hiyo.


Amesema ndani ya mwezi mmoja TAMISEMI itahakikisha inaanza kutatua changamoto hizo kisha akasisitiza usalama wa vifaa na vifaa tiba, pamoja na usajili wa vichanga ndani ya siku 90 baada ya kuzaliwa.


Prof. Nagu ametoa pongezi nyingi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mlimba na Menejimenti ya Sekta ya Afya kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa miundombinu ya afya, ukusanyaji wa mapato ya Hospitali, vifaa na vifaa tiba hali inayopelekea Halmashauri ya Mlimba kuwa na mazingira mazuri ya kazi kwa watumishi wa sekta ya afya.


Akiwa katika Hospitali ya Halmashauri, Prof. Nagu alikagua majengo mapya ya wodi za upasuaji, wodi za wanawake, wanaume, watoto na jengo la mama na mtoto. Mengine ni jengo la mionzi, maabara, jengo la huduma za wagonjwa wa nje na nyumba tatu kwa moja ya watumishi, iliyojengwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri.


Kando ya ukaguzi wa miundombinu na utoaji wa huduma, Prof. Nagu alipokea maoni kutoka kwa wanufaika wa huduma za afya katika Hospitali ya Halmashauri wakiwemo wajawazito na wagonjwa wa nje, kisha akawahimiza kujiunga na huduma ya Bima ya Afya kwa wote akisema huduma hiyo ndio muarobaini wa upatikanaji wa matibabu wakati wote.

Kwa aupande mwingine Prof. Nagu alitembelea Zahanati ya kijiji cha Mbingu ambapo pia alipongeza utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI katika Halmashauri ya Wilaya Mlimba imekuwa chachu kwa watumishi wa sekta ya afya na halmashauri kwa ujumla na hii imedhihirika katika maneno ya ufunguzi wa hotuba yake kwa watumishi wa sekta ya afya, na timu ya menejimenti ya halmashauri ambapo alisema,
“sisi tumekuja kuangalia huduma za afya, kuangalia mazingira yenu, kuwatia moyo na kuonja changamoto mnazozipitia katika uhalisia wake na kwa kweli tumefurahishwa sana na utendaji wenu. Kwa kweli mnastahili pongezi kubwa sana”.
Prof. Nagu katika ziara hiyo aliambatana na wataalamu kutoka wizarani kwake, mkoani, MSD, Bima ya Afya kwa Wote.

Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa