Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba, Ndg. Jamary Idrisa Abdul amefanya mazungumzo na Timu ya Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala Ngazi ya Mkoa baada ya kuwapokea Ofisini kwake leo asubuhi tarehe 17.10.2025.

Mkurugenzi Mtendaji ameishukuru timu hiyo kwa kusaidia kuasisi mauzo ya mazao ya biashara kwa mfumo wa stakabadhi za ghala ndani ya Halmashauri ya Mlimba ambapo mpaka sasa mazao manne; kakao, korosho, ufuta na mbaazi yanauzwa kwa njia hiyo, wakulima na halmashauri wananufaika.

Mbali na changamoto ikiwemo ya miundombinu ya barabara hasa wakati wa masika, Mkurugenzi Jamary ameiomba timu ya usimamizi wa mfumo wa stakabadhi za ghala ngazi ya mkoa kuliingiza shamba la korosho la halmashauri katika ushindani wa wazalishaji wakubwa unaoratibiwa na Bodi ya zao hilo nchini ili halmashauri iweze kunufaika zaidi kupitia zao hilo.

Kwa upande wake Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro, Ndg. Cesilia Sostenes amempongeza Mkurugenzi na wataalamu wake kwa usimamizi mzuri wa vyama vya ushirika unaobainika kupitia utulivu wa vyama hivyo kwani hakuna changamoto za malipo na wakulima wanaendela kuonesha imani kwa vyama vyao kwa kuendelea kukusanya na kuuza mazao yao kupitia vyama hivyo.


Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali, Dkt. Rosalia Rwegasira naye amempongeza Mkurugenzi na wataalamu wake kwa kufanya kazi kama timu na kuwaagiza wasimamie suala la ubora wa mbegu kwa wakulima ili kuweza kuongeza uzalishaji na kuimarisha zaidi uchumi wakulima na wananchi wa Mlimba kwa ujumla.

Pamoja na ahadi ya kushughulikia changamoto zilizo wasilishwa kikaoni hapo, ikiwemo ya miundombinu ya barabara na mabadiliko ya bei za mazao, kiongozi wa msafara huo ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Ndg. Beatrice Njawa amemtaka mkurugenzi kuwekeza katika ujenzi wa maghala ya mazao mchanganyiko katika kata zake ili kutatua changamoto ya uhaba wa huduma hiyo ndani ya halmashauri.


Pia ameitaka halmashauri kuanza kufikiria kupunguza kuuza mazao ghafi kwa kuyaongezea thamani huku akihimiza uongezaji ubora wa zao la kakao kwa kuzikausha kwa makaushio ya kisasa.
Timu ya Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala Mkoa wa Morogoro imeendelea kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa mfumo ndani ya halmashauri zake zenye kuzalisha mazao ya kimkakati ikiwemo Halmashauri ya Mji Ifakara, Halmashauri ya Wilaya Mvomero, Malinyi na Ulanga ili kujua changamoto na mafanikio yaliyokwisha kupatikana.


Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa