Pichani juu: waziri mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza na wakaazi wa wilaya ya Kilombero katika eneo la mchombe
SERIKALI imewahakikishia wakazi Wa Wilaya ya Kilombero kuwa itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Ifakara kuelekea Mlimba yenye urefu Wa kilomita 126.5.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati Wa ziara yake wilayani hapa na kusema kuwa ujenzi Wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami utawaondolea wananchi changamoto ya muda mrefu wa ubovu wa barabara hiyo hasa nyakati za masika.
Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuboresha miundombinu ya barabara nchini ikiwemo barabara hiyo inayobeba uchumi Wa wana Kilombero.
Waziri Mkuu aliyasema hayo baada ya wabunge watatu katika Wilaya hiyo akiwemo Wa Mlimba Susan Kiwanga,Mbunge Wa Kilombero Peter Lijualikali na Mbunge Wa Viti maalum Dk Gertrude Rwakatare kumuomba Waziri Mkuu kuwasaidia ili Barbara hiyo iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.
“Serikali imedhamiria kuimarisha barabara katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Ifakara-Mlimba kwa kiwango cha lami lengo likiwa ni kurahisisha usafiri pamoja na kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.”
Alisema Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya wananchi hivyo itajengwa na kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, hivyo aliwataka wananchi hao waendelee kuiamini Serikali yao.
Amebainisha ujenzi huo utakuwa Wa awamu tatu na awamu ya kwanza itakuwa kutoka Ifakara kwenda Mbingu na awamu ya pili kutoka Mbingu kuelekea Mlimba na awamu ya mwisho ni kutoka Mlimba kuelekea Njombe.
Alisema lengo la serikali ni kuona barabara zinakutanisha Mkoa kwa Mkoa zinatengenezwa na barabara hiyo itakutanisha Mkoa Wa Morogoro na Njombe na pia wanategemea kukutanisha Mkoa Wa Morogoro na Ruvuma kupitia barabara ya Malinyi-Namtumbo na kukutanisha Morogoro na Lindi kwa barabara ya Mahenge-Lindi.
Awali wabunge hao waliipongeza serikali kwa ujenzi Wa barabara ya Kidatu-Ifakara inayoendelea japo inasuasua hivyo kumuomba Waziri Mkuu kuiangalia pia barabara ya Ifakara-Mlimba ambayo huwa inasumbua Mara kwa Mara.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Morogoro, Jackson Mpankuli ahakikishe amepeleka walimu katika shule za msingi Mwangaza na Matangini zilizopo Mlimba ambazo zinakabiliwa na tatizo la upungufu wa walimu.
Waziri Mkuu alisema hadi Sepetemba 30 mwaka huu kiongozi huyo awe ameshawahashimia walimu katika shule. Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Suzan Kiwanga kulalamikia upungufu wa walimu.
Mbunge huyo alisema katika jimbo kuna tatizo kubwa la upungufu wa walimu hali inayosababisha baadhi ya wazazi kukodi walimu kwa ajili ya kuwafundisha Watoto wao, hivyo Waziri Mkuu aliagiza walimu wahamishiwe katika shule ndani ya wiki mbili.
Akizungumza wananchi katika eneo la Mchombe alikiwa njiani kuelekea Mlimba, Waziri Mkuu aliwataka wazazi, walezi na viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro kuhakikisha inadhibiti ongezeko la mimba kwa watoto wa shule.
“Lazima kuwalinda watoto wa kike ili wasipate mimba kwani watashindwa kuendelee na masomo, hivyo watashindwa kutimiza ndoto zao. Viongozi simamieni utekelezaji wa sheria kwa kuwachukua hatua wote waliowapa mimba wanafunzi.”
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro ambapo anatarajiwa kutembelea ya ulanga na kukagua miradi ya maendeleo ukiwemo mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya na kuzungumza na wananchi na watumishi.
Habari picha
pichani ni wakurugenzi wa Halmashauri ya Ifakara mji ndg Francis Ndulane (Kushoto) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero Injinia Stephano Kaliwa (kulia) wakimsikiliza waziri mkuu alipokuwa akiongea nao pamoja na watumishi wa Halmashauri zote mbili
Bwana John Mvanga aliyerejeshwa kazini na waziri mkuu baada ya kusimamishwa kazi tangu mwezi wa pili mwaka 2019, akimweleza jambo kiongozi huyo kwenye kikao baina ya watumihsi wa halmashauri mbili za ifakara na Mh. Kassim Majaliwa Jana.
Baadhi ya watumishi wa wilaya ya Kilombero waliojitokeza kumsikiliza waziri mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa katika kikao chake na watumishi hao
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa