Na, Milka Kaswamila- Mlimba DC
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mhe. Wakili Dunstan Kyobya, ameongoza kikao cha Baraza la Ushauri la Wilaya ya Kilombero na Kikao cha Kamati ya Sherehe ya Wilaya hiyo, vilivyo fanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mlimba uliopo katika Halmashauri ya Mji Ifakara.
Katika kikao cha Baraza la ushauri, wajumbe waliridhia kwamba jina la Jimbo la Kilombero libadilishwe na kuitwa Jimbo la Ifakara, barabara ya Mlimba-Uchindile ipandishwe hadhi kutoka TARURA kwenda TANROADS na kasi ya mradi wa maji wa Mlimba, wenye thamani ya shilingi bilioni 7.5 iongezwe ili wananchi waanze kunufaika na mradi huo.
Kwa upande wa Kamati ya Sherehe, mhe. Kyobya alizipongeza Halmashauri za Mlimba na Ifakara kwa kuwa katika tatu bora kimkoa kwenye matokeo ya mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka 2024, ambapo Halmashauri ya Mji Ifakara ilishika nafasi ya pili kimkoa na Halmashauri ya Mlimba ilishika nafasi ya tatu.
Mhe. Kyobya amezitaka Halmashauri hizo kuanza maandalizi mapema ili katika mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu 2025, ziweze kushika nafasi za juu zaidi kimkoa na kitaifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, mhe. Kyobya ameitaka Halmashauri ya Mlimba kutofautisha tozo za mpunga baina ya wakulima na wafanyabiashara, ambapo ametaka wakulima wanaolima chini ya tani moja wasikatwe ushuru.
Vilevile, ametumia vikao hivyo kuujulisha umma wa Kilombero kuhusu kushuka kwa gharama za kuunganishiwa umeme vijijini kutoka shilingi laki tatu hadi shilingi elfu 27 huku akiukumbusha umma kwamba hivi sasa Wilaya ya Kilombero imekuwa` Mkoa wa TANESCO wa Morogoro Kusini.
Katika kuhitimisha vikao hivyo, mhe. Kyobya amezitaka Halmashauri za Mlimba na Ifakara kuhakikisha mwaka huu wanasimamia vyema suala la utoro wa wanafunzi shuleni, utekelezaji wa shughuli za Lishe ndani ya Halmashauri, usimamizi wa masuala ya ukatili wa kijinsia, ugonjwa wa homa ya matumbo, na usimamizi wa uhifadhi wa mazingira huku akisisitiza kwamba hadi Juni 2025, kila Halmashauri kuhakikisha inapanda miche milioni mbili.
Vikao hivyo viwili vilihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, viongozi wa siasa, watendaji wa Kata za Halmashauri ya Mlimba na Ifakara, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Kilombero Wakurugenzi na wenyeviti wa Halmashauri hizo pamoja na wakuu wa Divisheni na Vitengo wa Halmashauri za Mlimba na Ifakara.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa