Pichani juu: mkuu wa wilaya ya Kilombero Chifu James Ihunyo (katikati) akizungumza na wakulima na wafugaji (Hawapo pichani) wakizungumzia kuhusu migogoro inayoendelea wilayani humo, pembeni yake niviongozi wengine.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Chifu James Ihunyo, amewataka wafugaji wote waliokuwa ndani ya Halmashauri hiyo, kuweka alama mifugo yao yote ili iweze kujulikana, kwa lengo la kutatua baadhi ya migogoro inayoendelea kuwepo baina ya wakulima na wafugaji.
Chifu Ihunyo ameyasema hayo leo, katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya Kilombero, ili kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, baada ya kuona ongezeko la mifugo mingi isiyotambulika, ambayo mwisho wa siku huishia kwenye migogoro mikubwa sana baina ya wakulima na wafugaji.
“Baada ya kikao hiki nawaomba wafugaji wote wajiandae,kwani mifugo isiyowekwa alama hatuitaki, maana matatizo ya migogoro yanazidi kuwa mengi na hii ni kutokana na malalamiko kuwa mengi sana, kutokana na ukweli kuwa kumekuwa na ongezeko la uvamizi wa wafugaji kutoka maeneo mengine kuhamia katika wilaya hii, kitendo kinachopelekea maeneo ya malisho kuwa machache hivyo kuingilia maeneo ya wakulima ambapo hapo, migogoro ndipo inapoanzia,”amesema chifu Ihunyo.
Naye katibu wa wilaya wa chama cha wananchi CUF ndg Bashiri Ally, amesema kwa upande wake ameona wafugaji ndio wanasumbua kwa kiasi kikubwa, kwani mazao ya wakulima yamekuwa yakiharibiwa na wafugaji, hivyo kupelekea hasara kwa wakulima wa mazao hayo.
Kwa upande wake Afisa ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero Abel Mbata, amesema kuwa, wanafanya jitihada kubwa za kuweka vibao kwa ajili ya mipaka, lakini matatizo yanaanzia vijijini kwani maeneo yanayotengwa hayatoshelezi kutokana kuongezeka kwa mifugo.
Aidha akielezea kwa mifano Afisa ardhi huyo amesema, katika kijiji cha Melela kuna ng’ombe elfu tatu, kwenye eneo la hekta Alfu mbili, ambayo ina sehemu ya malisho yenye hekta mia tatu, na kwa upande wa kijiji cha Msita kina jumla ya ng’ombe elfu saba, ambapo eneo lililopo ni hekta elfu tatu, yenye sehemu ya marisho hekta mia nne.
Katika hatua nyingine Diwani wa Signal Shema Ndama amesema, kamati za kulinda maeneo ziliundwa, lakini ziliingiliwa na viongozi wa Kijiji, hivyo katika kutoa rai yake, Mh. Shema amesema kuwa, anashauri wafugaji waachiwe walinde wenyewe maeneo yao ya malisho na wawe na mamlaka nayo, hivyo mamlaka kitendo ambacho kitatoa fursa kwa wao kama wamiliki wa eneo hilo kutotoa mwanya kwa wafugaji wengine kuhamia hapo kwani kitapunguza eneo la malisho yao.
Hata hivyo kwa upande wake Afisa mifugo na uvuvi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero Dr Aneth Kitambi amesema kuwa, hatua za ukaguzi wa mifugo na utoaji wa chanjo za homa ya mapafu kwa Wanyama, zimeanza kuchukuliwa kwani wameanza Signal na Kiberege, zoezi hilo litaendelea kwenye kata zote za Halmashauri ya wilaya ya Kilombero, huku akisema kuwa uzinduzi rasmi wa zoezi hili kwa kata zote, utafanyika Tarehe 19/8/2019 katika kata ya Signal.
Sanjari na hayo Dr. Kitambi ameongeza kuwa, idadi ya wanyama kwa kila mfugaji ipo, hivyo kila mtu ataangaliwa idadi ya mifugo yake, kwa kuwa kila mfugaji ana kadi yake ya utambuzi wa Wanyama anaomiliki, hivyo mfugaji atakayebainika kuwa na mifugo migi kupita kiwango, atapewa angalau miezi sita kupunguza nifugo hiyo, na kwa wale ambao hawana kabisa kadi ya utambuzi wa Wanyama anaowamiliki, huyo atahesabika kama mvamizi wa eneo hilo na kuchukuliwa hatua ikiwamo kufukuzwa kabisa katika
eneo hilo.
Habari picha: namna kikao hicho kilivyokuwa kinaendeshwa.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa