Na, Milka Kaswamila-Mlimba DC
Uzinduzi wa zoezi la utoaji wa mikopo ya asilimia kumi kwa vikundi vwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kwa Halmashauri ya Wilaya Mlimba, umefanyika jana tarehe 06.01.2024 kwa kishindo, huku Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, mhe. Wakili Dunstan Kyobya, akionesha uongozi bora kwa kukabidhi hundi ya mfano ya shilingi bilioni 2.2 na pikipiki 74 kwa vikundi vya walengwa wa mikopo hiyo.
Mkuu wa Wilaya, mhe. Dunstan Kyobya alikabidhi vitu hivyo akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mlimba, mhe. Innocent Mwangasa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilombero huku akisisitiza umuhimu wa mikopo hiyo katika kusaidia kukuza maendeleo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika Halmashauri na Wilaya kwa ujumla.
Awali, kabla ya kukabidhi hundi hiyo ya mfano pamoja na pikipiki, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mlimba, ndg. Jamary Idrisa Abdul alifafanua kuhusu mwenendo wa utoaji wa mikopo hiyo tangu mwaka wa fedha 2019/2020 Halmashauri hiyo ilipoanzishwa rasmi.
Mkurugenzi Jamary alisema licha ya changamoto ya baadhi ya vikundi kutorejesha kwa wakati ama kukwepa kabisa kurejesha mikopo wanayo chukua, vikundi vingi vimekuwa vikirejesha, na Halmashauri imekuwa ikiendelea kutoa mikopo kwa vikundi vya walengwa wa mikopo hiyo ambapo mwaka wa fedha 2019/2020 shilingi 400,000,000.00 zilikopeshwa na shilingi milioni 398,145,000.00 zilirejeshwa, mwaka 2020/2021 shilingi 950,670,000.00 zilikopeshwa na shilingi 950,167,000.00 zilirejeshwa.
Mwaka 2021/2022 shilingi 1,504,940,000.00 zilikopeshwa na shilingi 1,447,834,500.00 zilirejeshwa na mwaka wa fedha 2022/2023, shilingi 699,190,853.11 zilikopeshwa na shilingi 649,468,853.11 zilirejeshwa, na mwaka huu 2024/2025, Halmashauri imetenga shilingi 2,206,066,461.00 kwa ajili ya mikopo hiyo ambapo katika uzinduzi huo, jumla ya shilingi 746,795,000.00 zimeingizwa kwenye akaunti za vikundi 26 vya wanawake, 19 vya vijana na 4 vya walemavu.
Vikundi vya wanawake vimekopeshwa shilingi 388,000,000.00, vijana shilingi 330,795,000.00 na walemavu shilingi 28,000,000.00.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri, ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Jumuia za Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Morogoro, mhe. Innocent Mwangasa amevitaka vikundi vya walengwa wa mikopo hiyo kuhakikisha wanazingatia kaulimbiu ya utoaji wa mikopo hiyo “Rejesha kwa Wakati Nami Nikope” ili kutoa fursa kwa wananchi wengine wenye uhitaji wa mikopo, kuendelea kukopa na wao wenyewe kuendelea kuwa na sifa ya kukopesheka kwa awamu zingine mbeleni endapo watakuwa na uhitaji tena.
Nao wanufaika wa mikopo hiyo wamepaza sauti zao kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali mikopo hiyo itolewe katika Halmashauri zote nchini, ikiwemo Halmashauri ya Mlimba na wameahidi kuhakikisha wanarejesha kwa wakati ili wasiwanyime wengine fursa na kurudisha nyuma jitihada za Halmashauri na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, za kuwakwamua kiuchumi wananchi wake.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa