Na, Milka Kaswamila- Mlimba DC
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, mhe. Wakili Dunstan Kyobya, jana taerehe 06.01.2025, amekagua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari unaotekelezwa katika kijiji cha Namalumbo, Kata ya Igima kwa fedha kutoka Serikali Kuu, shilingi milioni 528.
Mhe. Kyobya, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri ya Mlimba fedha hizo na amependekeza kwa Kata ya Igima, kupitia kwa Diwani wao kwamba ikiwa wataona vyema, shule hiyo iitwe Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Pia, mhe. Kyobya amewapongeza mafundi wanaotekeleza ujenzi huo kwa kufanya kazi kwa kasi na kwa ubora kwani ujenzi wa shule hiyo ulianza mwanzoni mwa mwezi Novemba, 2024 na hivi sasa ujenzi upo katika hatua ya ukamilishaji.
Majengo yanayo jengwa katika mradi huo ni vyumba nane vya madarasa, jengo la utawala, maabara tatu za sayansi, maabara moja ya Jografia, maktaba moja, jengo la TEHAMA, na vyoo matundu 8.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Wilaya amempongeza Mkurugenzi wa Halamshauri ya Mlimba, ndg.Jamary Idrisa kwa usimamizi mzuri wa miradi, ikiwemo mradi huo kisha akamwagiza kuweka utaratibu mzuri ili ujenzi ufanyike usiku na mchana, ifikapo tarehe 15 ya mwezi huu shule zinapofunguliwa, shule hiyo ianze kutumika.
“Pia nataka wakati wa kufungua shule tarehe 15 tuzindue kampeni ya upandaji miti hapa na miti ambayo nataka tupande ni michikichi, mikokoa na mikarafuu. Lakini pia nataka migomba ya ndizi ipandwe shuleni hapa ili baadae ije kuwa chakula kwa wanafunzi” alieleza mhe. Kyobya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mlimba ambaye pia ndiye Diwani wa Kata ya Igima, mahali panapojengwa shule hiyo, mhe. Innocent Mwangasa, amemshukuru mhe. Mkuu wa Wilaya kwa ushirikiano mzuri katika usimamizi wa miradi na amesema uwepo wa shule hiyo unakwenda kuondoa utoro na adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shule, ambapo hivi sasa wanalazimika kutembea umbeali wa kilomita takriban saba kwenda shule ya Sekondari Mbingu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba ameahidi kuweka mazingira wezeshi ili kufanikisha ujenzi kufanyika usiku na mchana nao mafundi wanao tekeleza ujenzi huo, wamesema wako tayari kujenga usiku na mchana ili shule ikamilike kwa wakati tarajiwa.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa