Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mhe. Dunstan Kyobya amezindua mnada wa kwanza wa mtandaoni, wa Kakao ya wakulima wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba uliofanyika kwenye ghala la Chama cha Msingi cha Wakulima (AMCOS) lililopo kata ya Mbingu, tarehe 12.06.2024 asubuhi.
Katika mnada huo jumla ya kilo 43,750 za Kakao zimeuzwa kwa bei ya shilingi 25,720 kwa kilo, kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani unaoratibiwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).
Akizungumza na wananchi waliofika ghalani hapo kushuhudia mnada, mhe. Kyobya amehimiza wananchi kuongeza bidii katika kilimo cha mazao ya kimkakati ya mkoa wa Morogoro huku akiyataja kuwa ni Kakao, Karafuu, Chikichi, Kahawa, Pamba na Ufuta.
Vilevile, mhe. Kyobya amepiga marufuku ununuzi wa Kakao mbichi na usafirishaji wa zao hilo nje ya Halmashauri ya Mlimba kama halijapitia kwenye mfumo wa Serikali wa Stakabadhi Ghalani.
Amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu ye yote atakayebainika kukiuka maagizo hayo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba mhe. Innocent Mwangasa amesema kufanyika kwa mnada huo ni kutimia kwa ndoto ya muda mrefu ya Halmashauri kuwa na minada ya mazao mbalimbali ya biashara yanayo zalishwa ndani ya Halmashauri hiyo.
Amesema Halmashauri imetenga shilingi milioni 70 kwa ajili ya kununua miche ya Kakao ambayo itagawiwa bure kwa wananchi ili waweze kuiotesha kwenye mashamba yao.
Pia amesema wao kama Halmashauri wamejiandaa kuwapa elimu ya kutosha wakulima na amewaagiza maafisa ugani kuhakikisha wanamfikia mkulima mmoja mmoja na kuwapa elimu kwa vitendo ili watakapopata miche hiyo waweze kuiotesha na kuihudumia vizuri hatimaye ilete mavuno mazuri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba ndugu Jamary Idrisa Abdul amewapongeza wakulima kwa kujitokeza kushiriki mnada huo na kuahidi kuendelea kuhamasisha zaidi kilimo cha zao hilo ili mbeleni minada itakayo kuja ielete fedha nyingi zaidi kwa wananchi na Halmashauri kwa ujumla.
Naye mmoja wa wakulima wa Kakao Wilayani Mlimba, ndugu Calista John Ngasakwa amesema yeye pamoja na wakulima wenzake wamehamasika sana na mnada wa leo kwani kwa mara ya kwanza kabisa tangu waanze kulima Kakao, wameiuza kwa bei yenye tija kubwa (25,720), awali walikuwa wakiuza kilo moja ya Kakao kwa shilingi elfu 3,500 hadi 3,800.
Kupitia mnada wa leo, wakulima wameweza kupata jumla ya shilingi 1,125,250,000 na Halmashauri imepata shilingi 33,757,500, fedha ambayo kwa mujibu wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), inaingizwa moja kwa moja kwenye akaunti za wakulima na akaunti ya Halmashauri pia.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa