Tarehe 9 na 10 Januari 2026, Kamati ya kudumu ya Fedha, Uongozi na Utawala, ya Halmashauri ya Wilaya Mlimba imefanya ukaguzi wa miradi 12 ya maendeleo ya sekta za elimu na afya, katika kata za Masagati, Utengule, Kamwene, Mlimba, Mngeta, Igima, Namwawala na Idete, iliyotekelezwa katika kipindi cha Robo ya Pili ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 (Oktoba-Desemba).
Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Masagati, Utengule na Namwawala, pamoja na jengo la utawala, bwalo, na bweni moja katika shule ya sekondari ya wasichana ya Miembeni.
Aidha, Kamati ilikagua ujenzi wa bweni moja katika shule ya sekondari ya Matundu Hill, ujenzi wa shule mpya ya awali na msingi katika kijiji cha Ngajengwa, pamoja na ujenzi wa nyumba 15 za watumishi katika kitongoji cha Itongowa B.
Pia, ilikagua ujenzi wa wodi mbili za upasuaji na nyumba tatu za watumishi wa afya katika Hospitali ya Halmashauri, mradi ambao utafanya kazi ya utoaji wa huduma za afya kuwa bora zaidi.
Kamati imepongeza kasi na ubora wa utekelezaji wa miradi hiyo, ikisema kuwa utekelezaji huo unaonesha dhamira njema ya halmashauri kusogeza huduma za msingi karibu na wananchi wake.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba, Mhe. Martha Mkula, ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa kamati hiyo, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiletea halmashauri fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amefafanua kuwa miundombinu ya kisasa katika shule na vituo vya kutolea huduma za afya, pamoja na vifaa tiba vilivyopo, vinachangia kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi.
Pia kupitia ziara hiyo, Mhe. Mkula ameagiza watendaji wa kata zote kuanzisha “benki za matofali” kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa matofali wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu, wa Halmashauri ya Mlimba, Ndg. Filbert Mbwilo, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri wakati wa ziara hiyo, amesisitiza kwamba miradi yote iliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026, inatarajiwa kukamilika kwa wakati na kuanza kutumika.
Ziara ya Kamati ya Fedha, Uongozi na Utawala imefanyika kwa mafanikio makubwa, ikiwa ndio ziara ya kwanza tangu kuundwa kwa kamati hiyo mwezi Desemba 2025 baada ya kiapo cha udiwani, na inaonesha matumaini ya ushirikiano bora kati ya waheshimiwa madiwani na menejimenti ya Halmshauri.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa