SERIKALI kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Kilombero imeahidi kuwasaidia wanawake kupitia jukwaa la wanawake kwa kuwaunganisha na Taasisi na Asasi mbalimbali ili kuwapatia mafunzo yatakayosaidia kuwakomboa kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu katibu mkuu wizara ya elimu,sayansi na teknolojia Dk Ave Maria Semakafu wakati wa kongamano la jukwaa la wanawake wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero ambalo lilikwenda sambamba na maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo cha baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere yaliyofanyika katika Kijiji cha Msolwa Ujamaa wilayani hapa.
Dk Semakafu alisema amefurahishwa kuona jukwaa la wanawake linafanya kazi yake ipasavyo katika wilaya hiyo kwa kuwaunganisha wanawake katika kata zote na kusema kuwa dhana nzima ya majukumu ya wanawake ni kurejea misingi ya ujamaa.
Alisema katika kuwaunga mkono wanawake wa halmashauri hiyo atahakikisha wanapata mafunzo mbalimbali ya ujasiliamali na kwa kuanzia watawachukua wanawake wachache kwa ajili ya mafunzo na hao wachache wakirudi watakwenda kuwafundisha wenzao.
Hata hivyo naibu katibu mkuu huyo aliwaagiza wanawake hao kuhakikisha wanakaa na kujihudumia kiujamaa na pia wajitengenezee mitaji ili waweze kukopesheka sambamba na kuwachunga watoto wao wa kike wasipate mimba wakiwa mashuleni.
Awali mwenyekiti wa jukwaa la wanawake wilaya ya Kilombero Bi Amina Mrisho alitaja changamoto wanazokabiliana nazo wanawake wa wilaya ya Kilombero kuwa ni pamoja na kukosa elimu ya ujasiliamali, utambuzi wa fursa zilizopo maeneo yao, kukosa mitaji, uelewa wa sheria na haki zao na pia unyanyasaji wa kijinsia na mimba za utotoni.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero Dennis Londo alisema kuwa wao wameona umuhimu kuadhimisha siku hiyo katika Kijiji cha Msolwa Ujamaa kutokana na Hayati baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kushiriki kukiasisi Kijiji hicho kama Kijiji cha ujamaa cha mfano ambacho nacho bado kinasimamia falsafa ya baba wa taifa katika dhana ya ujamaa kwa kumiliki kwa pamoja mashamba makubwa na magari.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa