Pichani juu: Mhandisi Emanuel Kalobelo (mwenye suti Nyeusi) akizungumza na Dr. Annete Kitambi Afisa Mifugo na Uvuvi katika banda la Halmashauri ya wilaya ya Mlimba.
MAAFISA kilimo katika wilaya zote mkoani Morogoro wametakiwa kujiwekea malengo katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ili kuufanya mkoa huo kuwa kinara ya uzalishaji wa mazao hayo nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu tawala wa mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo wakati wa uzinduzi wa msimu wa kilimo kimkoa uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika kijiji cha Njage halmashauri ya wilaya ya Mlimba.
Akimwakilisha mkuu wa mkoa huo,Mhandisi Kalobelo amesema kwa kujiwekea malengo mkoa utajua wapi kuna tatizo na litatatuliwa vipi ili kuweza kumkomboa mkulima katika mazao anayolima na bila kufanya hivyo tutakuwa tunarudi nyuma kwani hatutakuwa na takwimu za kutosha.
Amesema kwa msimu huu wa kilimo ni muhimu kwa maafisa hao kilimo kuwakumbushia wananchi mazao gani yanafaa kwa kilimo na kwa wakati gani kwa kufanya tafiti mbalimbali za mbegu na mbolea na kwa kufanya hivyo watakuwa wamemwinua kiuchumi mkulima.
Amebainisha kuwa serikali ya mkoa huo ina mpango wa kuwakaribisha wataalamu wa utafiti wa udongo ili kubaini udongo wa maeneo mbalimbali yanafaa kwa kilimo cha aina gani lengo ni kujitathmini na kupiga hatua ya maendeleo katika maeneo yote mkoani humo.
Katibu tawala huyo pia amezikumbushia serikali za kata na vijiji kuhakikisha wanashirikiana na wataalamu wa kilimo kwa kupanga maeneo ya wakulima na wafugaji na hawatotaka kusikia migogoro ya wakulima na wafugaji.
Aidha katibu tawala huyo amezitaka halmashauri kuimarisha vyama vya ushirika ili iwe chachu katika maendeleo ya kilimo na pia wahakikishe pembejeo zote zinazohitajika zinakuwepo maeneo ya wakulima kabla ya uzalishaji.
Hata hivyo Mhandisi Kalobelo amewaomba wawekezaji kuwekeza mkoani humo ili kuweza kuchakata mazao mbalimbali na kumpatia faida mkulima wa mazao yake na kutaka maghala yote yaliyojengwa tokana na miradi mbalimbali yatumike na wawekezaji waanze kuweka mazao na sio kukaa bila mazao.
Kwa upande wao wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo wamemuahidi katibu tawala huyo kuhakikisha kuwa wanasimamia maelekezo ya serikali ili wakulima wake kupata mazao mengi na kufanya mkoa huo kuwa ghala la chakula.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa