Mkuu wa wilaya ya mvomero Mwalim Mohamed Utari amekabidhi rasmi mbio za mwenge wa uhuru 2017 kwa mkuu wa wilaya ya Kilombero Mh. James Ihunyo.
Awali kabla ya kukabidhi mwenge huo Utari alielezea kwa kifupi mbio za mwenge wa uhuru katika wilaya ya Mvomero zilipitia katika tarafa moja kati ya tarafa nne zilizopo wilayani mvomero ambapo aliitaja tarafa hiyo ni tarafa ya mvomero, aliendelea kufafanua kwamba mwenge ulikimbizwa katika kata moja kati ya kata 30 na kupitia vijiji viwili kati ya vijiji 130 vya wilaya ya mvomero, mwenge huo katika wilaya ya mvomero ulipitia miradi minane ambapo kati ya hiyo mitatu imewekewa mawe ya msingi, miwili imeonwa, mmoja umefunguliwa na miwili imezinduliwa.
Akielezea gharama za miradi hiyo Mh mkuu wa wilaya ya Mvomero amesema miradi yote iligharimu shilingi bilioni kumi na nne, milioni mia tisa sitini na tano, laki tano ishirini na saba elfu, mia tisa sitini na tisa na senti sabini na saba ambapo kati ya fedha hizo wananchi wamechangia jumla ya shilingi milioni mia moja kumi na tatu, laki mbili tisini na moja elfu, mia tatu hamsini , halmashauri imechangia shilingi milioni mia moja tisini na tano, laki moja na saba mia nane arobaini, serikali kuu imechangia shilingi bilioni kumi na nne, milioni mbili ishirini na saba, laki saba tisini na moja elfu, mia nane kumi na tisa na senti sabini na saba na wahisani wamechangia shilingi milioni mia nne ishirini na tisa, laki tatu thelathini na tisa, mia tisa sitini.
Baada ya kusoma taarifa hiyo fupi Mh. Utari ambaye ni mkuu wa wilaya ya mvomero alimkabidhi mkuu wa wa wilaya ya Kilombero magari na vifaa kwa ajili ya kukimbiza mwenge wa uhuru katika wilaya ya Kilombero, waratibu wa mwenge, gadi ya mwenge pamoja na wakimbiza mwenge wa uhuru sita wa kitaifa kwa mwaka 2017.
Wakimbiza mwenge wa uhuru kitaifa 2017 waliokabidhiwa ni Ndugu Fredrich Joseph Ndahani kutoka Singida, Ndugu Salome Obadia Mwakitalima kutoka Katavi, Ndugu Shukran Islam Suli kutoka Mjini Magharibi ambaye yupo kwenye kazi maalum, Ndugu Bahati Mwaniguta Lugodisha kutoka Geita, Ndugu Fatma Yunus Khassan kutoka Kusini Pemba, mwalimu wa wakimbiza mwenge mzee Khatibu khatibu bin khaji bin khaji, na kiongozi wa mwenge wa uhuru kitaifa ndugu Amour khamad Amour kutoka Kaskazini Unguja.
Akipokea mwenge wa uhuru Mkuu wa wilaya ya kilombero ndugu James Ihunyo kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Mvomero, alielezea kwa kifupi kwamba mwenge wa uhuru utakimbizwa katika tarafa mbili kati ya tarafa nne zilizopo Kilombero katika kata kumi kati ya kata 26 zilizopo katika halmashauri ya wilaya Kilombero.
Mkuu wa wilaya ya kilombero aliendelea kufafanua miradi mbali mbali ambayo itapitiwa na mwenge wa uhuru ambayo ni jumla ya miradi mitano yenye thamani ya shilingi bilioni mbili, milioni mia nne ishirini na tisa na mia tano sitini na tano na senti saba, aidha katika fedha hizo mchango wa serikali kuu ni shilingi bilioni mbili, milioni mia mbili tisini na tatu, laki tano arobaini na nane na senti thelathini na saba, pia michango ya wahisani ni milioni ishirini na tano, wakati halmashauri ya wilaya ya kilombero imechangia shilingi milioni thelathini, wakati michango ya wananchi ni shilingi milioni themanini na moja na elfu kumi na tano.Vile vile mkuu wa wilaya ya Kilombero katika taarifa yake alielezea kufurahishwa kwake na muamko wa wananchi na viongozi wa vyama mbalimbali kuweza kushiriki kwa pamoja katika kuupokea mwenge wa uhuru.
Mh Ihunyo aliwahakikishia ulinzi na usalama wakimbiza mwenge wa uhuru kitaifa kwa kipindi chote watakapokuwepo ndani ya halmashauri ya wilaya ya Kilombero na kutamka rasmi uzinduzi wa mbio za mwenge wa uhuru ndani ya halmashauri ya wilaya ya kilombero.
Baada ya mkuu wa wilaya ya kilombero kutoa taarifa fupi,alimkaribisha kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa ndugu Amour khamad Amour ili aweze kuzungumza na wananchi wa wilaya ya kilombero.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa alianza kwa kuwashukuru wananchi waliojitokeza kuupokea mwenge wa uhuru, na kueleza madhumuni ya kuanzishwa na kuenziwa kwa mwenge wa uhuru katika taifa kama vile kuleta amani, kuuondosha chuki, dharau kuleta upendo na maendeleo katika taifa letu, pia alieleza kuwa mwenge wa uhuru utakimbizwa katika mikoa 31 ya Jamuhuri ya muungano waTanzania, halmashauri 195 za Jamhuri ya muungano wa Tanzania, ukihamasisha na kuchajiisha maendeleo, umoja, upendo, utulivu, uzalendo, na uchapakazi kwa watanzania wote.
Vilevile kiongozi wa mbio za mwenge alieleza kuwa mwenge wa uhuru kutofungamana na upande wowote, kwa kuwa shughuli kubwa ya mwenge wa uhuru ni kuzindua miradi mbalimbali inayoratibiwa na wilaya husika na kuwekewa mawe ya msingi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wote kwa usawa na pasipo upendeleo wa itikadi yeyote ile.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa aliendelea kuwaeleza wananchi kauli mbiu ya mwenge wa uhuru kwa mwaka 2017 ambayo inaendana na kauli mbiu ya serikali ya wakati huu kuwa ni "Shiriki kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu".
Kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa amewaeleza wananchi umuhimu wa sekta ya kilimo katika uzalishaji wa malighafi ambazo zitatumika viwandani na kusisitiza kuendeleza na kudumisha sekta ya kilimo. Aliwaeleza wanachi umuhimu wa viwanda katika kukuza uchumi wa nchi yetu akitolea mfano mataifa mengi yalioendelea duniani kuwa yalifanya hivyo kupitia maendeleo ya viwanda, hivyo kusisitiza uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo na vya kati kwa maendeleo ya Taifa letu ilikuendana na kauli mbiu ya serikali yetu ya awamu ya tano.
Akitembelea kikundi cha kinamama wanaoishi na virusi vya ukimwi Kidatu kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa amesisitiza agizo la serikali kuitaka kila halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake ambapo asilimia 5 iende kwa vikundi vya kinamama na asilimia 5 iende kwa vijana huku akishukuru sana kwa kukiona kikundi hicho cha wakinamama wanaoishi na virusi vya ukimwi huku akielezea watu wanaoishi na virusi vya ukimwi ni sehemu ya taifa letu na wanapaswa kupewa fursa mbalimbali za kukuza uchumi wa taifa bila unyanyapaa, wakati huohuo kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa ameelezea dhamira ya serikali katika mapambano dhidi ya virusi vya ukimwi ni kuhakikisha Tanzania inaendelea bila virusi vya ukimwi, unyanyapaa na bila vifo vinavyotokana na virusi vya ukimwi.
Aidha wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa miundombinu ya maji katika kata ya Msolwa station kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa alikagua tenki la maji linalojengwa leje ukubwa wa ujazo wa lita elfu 90 ambapo jumla ya vituo 39 vya maji vitajengwa ili kukidhi mahitaji ya wananchi, mradi huu wa maji utawanufaisha jumla ya wananchi 8756 ambao watapata huduma ya maji, mradi umegharimu jumla shilingi bilioni mbili, laki mbili themanini na nane elfu, mia sita na tatu na senti thelathini na saba ambazo zimetolewa na serikali kuu na wahisani.
Akihutubia wananchi wa msolwa station kwa niaba ya kiongozi wa mbio za mwenge Ndugu Fredrick Joeph Ndahani hakusita kuonyesha hofu yake katika ukamilishwaji wa mradi huo kutokana na muda mchache uliobaki kabla ya mradi huo kukabidhiwa teyali kwa matumizi baada ya mradi huo kubakiza siku chache kabla ya kukamilika hali ya kuwa mpaka sasa ujenzi wake ukiwa umekamilika kwa asilimia 45 tu, aliwataka wananchi waufuatilie mradi huo na kuhakikisha mradi unakamilika kwa siku hizi chache teyali kwa kutoa huduma na ikiwa haujamilika wasisite kutoa taarifa kupitia namba 113.
Miradi mingine iliyoonwa na mbio za mwenge wa uhuru 2017 ni pamoja na kikundi cha wajasilimali cha ufugaji nyuki cha juhudi kata ya Man'gula "A" chenye idadi ya mizinga 67 kati ya hiyo mizinga 14 ni ya kienyeji, 6 ni ya kibiashara na mizinga 47 ni ya kisasa, kikundi cha wafugaji nyuki kiliwezeshwa na halmashauri ya wilaya ya Kilombero kiasi cha shilingi milioni tano ikiwa ni mchango kutoka Halmashauri.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru pia alizindua mradi wa chumba cha upasuaji (thaeatre room) katika kituo cha afya Mang'ula ambapo ujenzi huo ulianza january 2017 na unatarajiwa kukamilika mwisho wa mwaka huu 2017, mradi umefikia hatua ya kupauliwa, kuezeka na kupigwa ripu. Jumla ya shilingi milioni 88 zinatarajia kutumika kukamilisha ujenzi wa mradi ambapo mpaka sasa jumla ya shilingi milioni 44 teyali zimekwishatumika ambapo kati ya hizo milioni 44 mchango wa wananchi ni shilingi milioni 14 na Halmashauri imechangia shilingi milioni 30. Jumla ya wanachi 36,176 watafaidika na mradi huo pindi utakapokamilika, sambamba na uzinduzi huo ugawaji wa vyandarau vya kujikinga na mbu waambukizao malaria ulifanyika kwa kuwapatia kina mama wajawazito jumla ya vyandarua kumi.
Shughuli za utunzaji wa mazingira kwa kutumia majiko banifu yenye kutumia mabaki ya randa za mbao, makaratasi, mabaki ya mkaa na majani ya muwa ni moja ya kazi ambazo kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru 2017 Mh. Amour Hamad Amour alizitembelea na kuziona jinsi zinavyofanya kazi katika viwanja vya hotel ya Twiga kata ya Mang'ula ''A'', aidha Bi Fatuma Abeid ambaye ni katibu wa kikundi hicho alitumia nafasi hiyo kuomba kusaidiwa vitendea kazi ili kuongeza ufanisi wa kazi zao jambo ambalo lilipokelewa na kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa ambapo alimuagiza afisa maendeleo ya jamii Kilombero Bi Loyce Mnyenyelwa kuhakikisha anawawezesha wanakikundi hao haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wake afisa maendeleo ya jamii Kilombero alimuhakikishia kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa kuwa teyali kikundi hicho kipo kwenye bajeti ijayo ya 2017/2018 ambapo kitawezeshwa kutoka halmashauri ya wilaya ya Kilombero, na wakati huohuo kikundi cha SILC ambacho kinajihusisha na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali kwa kutumia rasilimali asilia kama vile majani ya mgomba nacho kilionyesha bidhaa zake mbalimbali kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru 2017 ambapo kilimueleza kiongozi huyo kwamba soko lao kubwa ni Italia ambapo wafadhili wao wanapatikana huko.
Mradi wa ujenzi wa vyoo vya kisasa vya wanafunzi katika shule ya msingi Darajani nao ulizinduliwa na mbio za mwenge wa uhuru 2017 ambapo mradi huo ulianza mwezi wa tatu mwaka 2017 na unatarajia kukamilika mapema mwezi wa saba mwaka 2017, mradi wa vyoo hivyo utakidhi mahitaji ya wanafunzi 837 ambao watapata huduma bora na ya kisasa ya vyoo, hadi kufikia sasa awamu ya kwanza ya majengo ya vyoo hivyo imeshakamilika ambapo awamu ya pili itakuwa ni kupiga rangi vyoo hivyo na kumalizia kazi ndogondogo za kukamilisha ujenzi, jumla ya shilingi milioni 39 laki moja na elfu hamsini zitatumika ili kukamilisha ujenzi wa mradi ambapo kati ya fedha hizo wananchi wamechangia shilingi milioni kumi na nne laki moja na hamsini elfu, wahisani wamechangia shilingi milioni ishirini na tano. Faida za mradi ni kuwawezesha wanafunzi kupata eneo safi la kujisaidia, na kupunguza magonjwa ya mlipuko kwa wanafunzi. Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru 2017 alipongeza jitihada za ujenzi wa vyoo hivyo ambavyo vinajali makundi ya watu wote wakiwemo walemavu pamoja na kujali umuhimu wa mahitaji ya jinsia ya kike, vilevile amewapongeza wananchi kwa kujitoa kwao kwa kuchangia ujenzi wa vyoo hivyo huku akiwasisitiza wananchi kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi, rushwa, ugonjwa wa malaria pamoja na matumizi ya madawa ya kulevya.
Katika kukamilisha uzinduzi wa miradi mbio za mwenge wa uhuru 2017 zilizindua mradi wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao lenye mashine ya kumenya mpunga mjini kiberege, mradi ambao umetekelezwa na mkazi wa kijiji cha kiberege Bwana Mahmoud Hamduni ambapo lengo la mradi huo ni kuhifadhi mazao ya wakulima baada ya kuvuna, mradi pia una mashine za kukoboa mpunga teyali kwa soko la biashara kutoka kwa wakulima. Mradi hadi kukamilika kwake umegharimu shilingi milioni hamsini na mbili, laki mbili thelathini na mbili elfu ambapo kati ya fedha hizo shilingi milioni thelathini na sita na elfu thelathini na mbili ni ujenzi wa ghala na shilingi milioni kumi na sita laki mbili ni ununuzi wa mashine ya kukoboa mpunga na vifaa vya kuhifadhia mpunga.
Katibu tawala wilaya ya Kilombero Bwana Selasela alihitimisha mbio za mwenge wa uhuru 2017 katika viwanja vya shule ya msingi kiberege kwa kusoma risala ya utii ya wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero, ambapo katika risala hiyo alitanabaisha kwamba wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero bado wanazingatia mahudhui ya kuwashwa mwenge wa uhuru ili uweze kumulika ndani na nje ya mipaka yetu, ulete matumaini mahali ambapo hakuna matumaini, upendo palipo na chuki na heshima palipo na dharau.
Baada ya risala ya utii Mkuu wa wilaya ya Kilombero Mh. James Ihunyo alikabidhi risala ya utii kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa 2017, Bwana Amour Hamad Amour ambapo kwa heshima alikiri kupokea risala ya utii ya wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero na kuahidi kuikabidhi kwa Mh. Dr John Pombe Joseph Magufuli raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania huku akimuomba mwenyezi mungu amsaidie.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa