Na, Milka Kaswamila-Mlimba DC
Halmashauri ya Wilaya Mlimba inajivunia maendeleo makubwa ambayo inaendelea kuyatekeleza katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, elimu ya awali, msingi, sekondari, na kwa kuendelea kuhakikisha utekelezaji wa miradi unafanyika kwa viwango vya juu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mlimba, ndg. Jamary Idrisa Abdul amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi inayoendelea kutekelezwa ndani ya Halmashauri hiyo.
Katika ziara hiyo, amekagua miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Zahanati ya Chiwachiwa, ujenzi wa wodi tatu katika Hospitali ya Halmashauri, ukamilishaji wa wodi tatu za upasuaji, ujenzi wa nyumba tatu kwa moja za watumishi wa afya na ujenzi wa shule mpya ya sekondari katika Kata ya Igima, huku akitoa maelekezo ya kuboresha na kuhakikisha utekelezaji wa miradi unaendelea kama ilivyo pangwa.
Aidha, Mkurugenzi Jamary ameeleza kuridhishwa na jitiihada zinazofanywa na mafundi pamoja na wasimamizi wa miradi hiyo, za kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora na kwa haraka, huku akisisitiza umuhimu wa usimamizi mzuri na uwazi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Kwa sasa Halmashauri ya Mlimba tunatekeleza miradi nane katika sekta ya elimu ya sekondari, miradi 27 sekta ya elimu ya awali na msingi, na miradi 13 katika sekta ya afya.
Vilevile, Halmashauri ilitenga shilingi 100,000,000.00 kutoka katika mapato yake ya ndani ili kutengeneza viti na meza 1,818 kazi ambayo inatazamiwa kukamilika hivi karibuni ili Januari 2025 shule zitakapo funguliwa, samani hizo ziweze kutumika shuleni.
Miradi hii ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa Halmashauri ya Mlimba na tutahakikisha kwamba kila mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kwa maslahi ya jamii. Sisi Halmashauri pamoja na Serikali Kuu, tunalenga kuboresha maisha ya wananchi wetu kwa kutoa huduma bora na miundombinu imara" alieleza kwa kina Mkurugenzi Jamary.
Halmashauri ya Wilaya Mlimba inaendelea kufanya juhudi za kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na inakuwa na manufaa kwa jamii, ikiwa ni sehemu ya harakati za serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha maisha ya wananchi.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa