Pichani juu: Mkuu wa wilaya ya Kilombero Ndg James Ihunyo (Mwenye shati la kitenge la orange) akiwaonyesha wananchi kupitia ramani iliyopo kwenye simu yake, eneo la mpaka wa pori tengefu la Kilombero.
Mkuu wa wilaya ya Kilombero Ndg James Ihunyo, jana amefanya ukaguzi wa mipaka yote inayolalamikiwa ya pori Tengefu la Kilombero, ili kujiridhisha kutokana na malalamiko ya wananchi wa kijiji cha Idandu, ambao wameiomba serikali iwaongezee eneo kutoka katika eneo hilo.
Wananchi hao wanadai kuwa ni eneo lao pekee, ndilo mpaka wake una eneo dogo sana ukilinganisha na vijiji vya Mofu na Kalenga, ambapo wao wanaonekana wapo kwa mbele zaidi ya kijiji cha Idandu
Hata hivyo Ndg Ihunyo aliwaeleza kuwa, Tayari watendaji kutoka katika idara ya Ardhi ya wilaya ya Kilombero, wamekwishafanya busara ya kutosha sana, kwani tayari wamewasaidia kwa kuwaongezea zaidi ya kilometa moja na nusu kutoka katika mpaka wa mkuruza wa okoa bonde na kuongeza kuwa si cha mita miatano tena mbele ili kuweza kufikisha ukubwa wa kilometa mbili, hivyo wao kama wananchi wanatakiwa kuishukuru sana serikali, hususan watendaji hao wa Ardhi kwani laiti kama angekuwa yeye asingeweza kuwa na ujasiri huo wa kuweza kuongeza hata mita mbili.
Pamoja na hayo, bado Ndg Ihunyo amesisitiza kuendelea kuwasaidia wananchi hao wa kijiji cha Idandu kwa kuwaomba waendelee kuwa watulivu kwani tayari mipaka amekwishaiona, na atapata nafasi ya kwenda kuiona mipaka mingine ya eneo linalolalamikiwa na wananchi hao la msitu wa Namwai na kuja na majibu sahihi ya namna ya kuweza kuliendea suala hilo kwa mipaka yote katika sehemu hizo mbili, siku ya Alhamisi ya tarehe 6/12/2018 kwenye majira ya saa nane mchana,atakapokutana na wananchi hao, kwenye kijiji hicho cha Idandu ili wananchi wapate kusikia kitakachoamuliwa na serikali, kwa maslahi yake na wananchi kwa ujumla.
Aidha amewataka wananchi wote ambao wanamiliki maeneo makubwa, yaliyo zaidi ya heka hamsini wayarudishe kijijini kwani hao ndio wanaosababisha upungufu wa maeneo, na wanakijiji wengine kukosa maeneo kwa kuhodhiwa na watu wachache, hali ambayo inapelekea wananchi hao kuomba maeneo mengine ambayo hayahitajiki kupewa wananchi, kama inavyotokea katika eneo hilo la kijiji cha Idandu.
‘’Tatizo kubwa linalofanya ninyi wananchi kuiona serikali haitaki kusikiliza maombi yenu juu ya kuongezewa vipande vya ardhi mnavyovitaka ni kuwa, kuna baadhi ya wenzenu wanamiliki zaidi ya heka mia tano, kitu ambacho kwa mujibu wa sheria za umilikaji ardhi vijijini, ni kinyume na sheria, kwani mwisho wa kumiliki ardhi kwa sheria za vijiji ni heka Hamsini na ikiwa itazidi hapo, ni lazima wizara ya Ardhi ihusishwe.’’ Alisema.
Ndg Ihunyo amesema kuwa, serikali ya wilaya ya Kilombero imefanya uainishaji mpya wa mipaka, ambapo vijiji zaidi ya 23 vimehusishwa, ili kuweza kuyalinda maeneo yote ambayo ni hifadhi za taifa iwe mapori au hata Ardhi tepetepe, kwaajili ya maslahi ya Taifa kwa ujumla.
Nao wananchi wamesema kuwa wamekubaliana na maagizo ya mkuu wa wilaya na kusema kuwa wamekwishaona njia ya utatuzi wa matatizo yao, pamoja na hayo wameahidi kushirikiana na serikali ya wilaya ya Kilombero, ili kuweza kuhakikisha kuwa kila mmoja anapata maeneo ya kufanyia shughuli zake za kimaendeleo.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa