Pichani: Mkuu wa wilaya ya Kilombero Ndugu James Ihunyo, akizungumza na wanakijiji wa kata ya Namwawala.
MKUU Wa wilaya ya Kilombero James Ihunyo, amesema kuwa ndani ya wilaya hiyo kama kutatokea magonjwa ya kujitakia ya mlipuko, basi kiongozi Wa eneo husika lazima achukuliwe hatua.
Ihunyo ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati akizungumza na wananchi sambamba na kulitambulisha shirika jipya lisilokuwa la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya Afya na usafi wa mazingira la HAPA, katika kata ya Namwawala wilayani humo.
Mkuu huyo Wa Wilaya amesema, ni aibu kwa kiongozi katika eneo lake kutokea magonjwa ya milipuko kama kipindupindu ama kuhara na kusema kuwa, magonjwa hayo ni ya kujitakia na yanazuilika pale kiongozi atakapotimiza wajibu wake katika usafi.
"Kusikia eti kijiji ama kata kuna mlipuko Wa kipindupindu ni aibu, kwani ugonjwa huo unazuilika kwa kuweka mazingira safi ikiwemo kuwa na choo bora, sasa ukisikia mlipuko umetokea basi ujue kiongozi huyo hafai, kwani hakuwasimamia wananchi wake katika suala la usafi Wa mazingira " alisema.
Amewaagiza viongozi kuanzia ngazi ya vitongoji kufanya ukaguzi Wa Mara kwa Mara, kuhusu usafi katika kaya zinazowazunguka ikiwemo vyoo bora na familia yeyote isiyo na choo, ikamatwe na kupelekwa katika vyombo vya Sheria.
"Mlipuko Wa magonjwa ya kuhara na kipindupindu yanatokana na uchafu unaotokana na kula kinyesi, nanyi Sheria ndogo mnazo kwa nini hamzitumii watu kuwakamata ama kuzuia kujisaidia ovyo bila kuwa na choo?" Alihoji.
Amesema hapendi kuona hali iliyopo hivi sasa kwa asilimia 80 ya wagonjwa wanaoenda hospitali, kuonekana wanaugua magonjwa yanayotokana na tatizo la uchafu, ikiwemo kipindupindu na kuhara.
Mkuu huyo Wa Wilaya amesema, katika kuhakikisha hayatokei magonjwa ya kujitakia ya mlipuko katika Wilaya hiyo, amewaagiza watendaji kuanzia ngazi ya vijiji na kata, kuandaa mashindano ya usafi wa mazingira na choo bora na washindi kupewa zawadi mbalimbali na hiyo itahamasisha kila Mwananchi ndani ya Wilaya hiyo, kuwa na choo bora na kuwa na mazingira bora.
Naye Afisa Afya katika halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Mbonja Kasembwa alisema kuwa, halmashauri kwa kushirikiana na shirika la HAPA wamefanikiwa kutembelea Wilaya nzima, na kuhamasisha suala LA mazingira na ujenzi Wa vyoo bora na asilimia 80 ya wananchi wake kwa sasa wana vyoo bora.
Katika hatua nyingine, Meneja mradi Wa shirika la HAPA Baraka Mwakubali amesema, mradi huo toka uanze mwaka Jana kwa kushirikiana na halmashauri umekuwa na mafanikio makubwa, ila ametoa ushauri kwa vijiji ambavyo mazingira yake ni safi, na kaya kuwa na choo vianze mchakato Wa kuhamasisha kaya zijenge vyoo bora vya kisasa.
Mwakubali amesema kwa vijiji ambavyo kaya zake hazina vyoo, viendelee kuhamasisha ujenzi Wa vyoo pamoja na kutumia Sheria ndogondogo za vijiji, katika kuhakikisha kaya zinajenga vyoo na pia viongozi junamosi ya mwisho wa mwezi, wakague hali ya usafi Wa mazingira na ujenzi Wa vyoo, pamoja na uwepo Wa vifaa vya kunawia mikono vyenye Maji na Sabuni.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa