BAA la uharibifu wa mazao limejitokeza katika wilaya ya Kilombero baada ya panya waharibifu wa mazao kushambulia mazao ya mpunga na mahindi na kusababishia hasara wakulima.
Panya hao wameanza uharibifu huo tokea Novemba mwaka jana ambapo walianza kuonekana katika kata za Mwaya na Mngeta katika halmashauri ya wilaya ya Kilombero na kisha kuonekana katika kata nyingine katika halmashauri zote mbili za Kilombero na mji wa Ifakara.
Hata hivyo juhudi za halmashauri hizo mbili katika kuwadhibiti panya hao zilifanikiwa ambapo halmashauri hizo ziliamua kununua sumu na kuweza kuwateketeza panya hao japo kuna baadhi ya maeneo bado wanaendelea kusumbuliwa na wadudu hao waharibifu.
Mkurugenzi wa mji wa Ifakara Francis Ndulane alisema baada ya kupata taarifa mapema mwezi huu aliamua kuwasiliana na mkurugenzi mwenzie wa wilaya na kuelezwa kuwa tatizo hilo lilianzia katika halmashauri hiyo kwa mashamba ya mahindi kuharibiwa katika kata ya Chita.
Ndulane alisema lakini siku chache alipewa taarifa kuwa maeneo jirani na halmashauri yake huko Idete wamevamia panya hao na baadae kusambaa katika vijiji viwili vya halmashauri yake ambavyo ninIhanga na Lumemo.
Alisema baada ya kubaini uvamizi huo katika halmashauri yake walipanga mkakati na halmashauri ya wilaya ya Kilombero ili kuweza kuwadhibiti panya hao na kupeleka taarifa mkoani na baadae kuamua kununua sumu ili kuweza kuwaangamiza panya hao.
Mkurugenzi huyo wa mji alisema katika ununuzi wa sumu hiyo halmashauri ya wilaya Kilombero walinunua kilo 50 na halmashauri ya mji walinunua kilo 10 na kazi ya usambazaji wa sumu hiyo ulianza na maeneo mengi katika halmashauri ya mji wamefanikiwa kuwaangamiza panya hao.
Ndulane alisema kwa sasa wataalamu wa kilimo katika halmashauri hiyo wamesambaza sumu maeneo yote yaliyoathirika na pia wanahamasisha wakulima kutumia njia za kienyeji ili kuwadhibiti panya hao ambapo kwa namna moja ama nyingine wamefanikiwa.
Naye Afisa Kilimo,Umwagiliaji na Ushirika wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero Mohamed Ramadhani alisema kwa sasa hali ni shwari katika maeneo mengi wilayani humo kwani waianza kugawa sumu toka Januari 6 mwaka huu na tatizo hilo lilianza kubainika wilayani humo toka Novemba mwaka jana.
Ramadhani alisema ekari zaidi ya 300 zimeharibiwa na panya hao na kubainisha kuwa licha ya kusambazwa kwa sumu katika maeneo yaliyoathirika pia mvua zilizoanya kunyesha hasa maeneo ya mabondeni zimesaidia kuua panya hao ambapo kwa hivi sasa wataalamu wanaendelea kutembelea maeneo mbalimbali ili kuwamaliza kabisa panya hao.
Mwisho
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa