Maonesho ya Wakulima (Nanenane) Kanda ya Mashariki yamezinduliwa leo tarehe 02.08.2024 na Mkuu wa Mkoa wa Tanga mhe. Batilda Burian, kwenye Uwanja wa Mwalimu Nyerere Nanenane Morogoro.
Akizungumza na hadhira iliyo kuwepo wakati wa uzinduzi huo, mhe. Batilda amewaalika wafugaji waje kwenye maonesho wajifunze aina za malisho ambayo yanaweza kulimwa kwenye eneo dogo lakini yakalisha mifugo mingi.
Mhe. Batilda amesema elimu hiyo itasaidia wafugaji kuweza kufuga kisasa na kuepuka ufugaji holela wa kuhamahama ambao unachangia sana kuwepo kwa migogoro kati ya wakulima na wafugaji pindi mifugo inapoingia kwenye mashamba ya wakulima na kula mazao.
Vilevile, mhe. Batilda amepongeza Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) pamoja na wanafunzi wake walio gundua na kutengeneza application ya kutambua afya ya mnyama mmoja mmoja wawapo bandani.
“Hongera sana SUA na vijana wetu kwa kugundua hilo na tunaomba mpite kwenye maeneo yetu kuzungumza na wafugaji wetu kuhusu teknolojia hiyo” alieleza mhe. Batilda.
Kwa upande wa kilimo, mhe. Batilda amemshukuru Rais Samia kwa kuwezesha maafisa ugani wa Halmashauri zote nchini kupata pikipiki na vyombo vya kupima afya ya udongo ili kuimarisha shughuli za kilimo kwenye maeneo yao ya kazi.
Pia, mhe. Batilda amewataka wakulima wajifunze na kubadilisha aina za kilimo kwa kufanya kilimo cha umwagiliaji, vitalu nyumba na ufuatiliaji wa teknolojia za kisasa ili waweze kujikomboa zaidi kiuchumi.
Mhe. Batilda amesema mikoa ya Kanda ya Mashariki (Pwani, Morogoro, Dar-es-Salaam na Tanga) ina kila sababu ya kufanya vizuri zaidi katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya masuala ya kilimo mifugo na uvuvi kwa sababu Taasisi za Tafiti za sekta hizo zimo ndani ya kanda hiyo kama vile SUA Morogoro, TARIRI Tanga na Taasisi ya tafiti za uvuvi huko Kunduchi Dar-Es-Salaam.
Akizungumzia Kauli Mbiu ya Maoenesho ya Nanenane ya mwaka huu, mhe. Batilda ametoa wito kwa wakulima, kushiriki kikamilifu kujitokeza kugombea na kuchagua viongozi bora watakao himiza shughuli za kilimo.
“Kiongozi ni lazima aoneshe mfano ili wananchi wake waweze kujifunza kutoka kwake” alisema mhe. Batilda.
Aidha, mhe. Batilda amesema sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi zimetoa ajira kwa zaidi ya asilimia 65, zimechangia pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 28 na zinachangia usalama wa chakula na lishe bora kwa wananchi.
Ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha miundombinu ya sekta hizi ikiwemo kuanzisha skimu za umwagiliaji, kuanza kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za ufugaji, kuimarisha Benki ya Kilimo na miundombinu ya usafiri na usafirishaji.
Kauli Mbiu ya Maonesho ya Nanenane mwaka huu inasema “Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa