Tarehe 25.06.2024 jioni, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekabidhi kwa Kampuni ya Uhandisi kutoka China, (China First Highway Engeneering Company) mradi wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ijulikanayo kama Mbingu-Chita JKT.
Makabidhiano hayo yamefanywa na Mratibu wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya TANROADS mkoa wa Morogoro mhandisi Geofrey Mutakubwa akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba ndugu Jamary Idrisa, huko Mbingu.
Mhandisi Mutakubwa amesema ujenzi wa barabara ya Mbingu- Chita JKT yenye urefu wa kilomita 37.5 unatazamiwa kufanyika kwa kipindi cha miezi 20 kuanzia tarehe 25.06.2024 na fedha za utekelezaji wa mradi huo zimetolewa na Serikali ya Tanzania inayo ongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Mradi huu unagharimu shilingi bilioni 70.8 pesa ya Tanzania na pesa yote imetolewa na Serikali ya Tanzania pekee, hivyo watanzania na hasa wananchi wa Mlimba hatuna budi kuishukuru sana Serikali kwa jambo hili makini sana” alieleza Mutabuka.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba ndugu Jamary Idrisa amesema ujenzi wa barabara hiyo utakapo anza utaamsha ari ya wawekezaji kuja kuwekeza Mlimba hasa kwenye sekta ya kilimo ambayo ndio uti wa mgongo wa Halmashauri hiyo.
Pia, ndugu Jamary ameahidi kuwapa ushirikiano wa karibu wahandisi kutoka China wanaotekeleza mradi huo ili kuhakikisha wanaukamilisha kwa wakati.
Naye kiongozi wa timu ya wahandisi hao kutoka China amemshukuru Mkurugenzi Jamary kwa mapokezi mazuri na amempongeza kwa kuwa na Ofisi nzuri katika eneo lenye mandhari nzuri.
“Nimependa sana mazingira ya mahali hapa” alisema kiongozi huyo.
Kwa muda mrefu wananchi wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba wamekuwa wakiisihi Serikali kujenga barabara ya lami kwenye Halmashauri yao ili waondokane na adha ya usafiri hasa kipindi cha masika ambapo barabara zimekuwa zikiharibika sana na kusababisha wananchi kushindwa kutoka ama kuingia kwenye maeneo mbalimbali ya Halmashauri hiyo.
Ni hakika kuanza kwa ujenzi wa barabara ya Mbingu-Chita JKT kutaamsha furaha na tabasamu mioyoni mwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba kwani suala la kuwa na barabara nzuri na imara ni kiu na shauku yao ya muda mrefu.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa