Uandikishaji wa wanafunzi shule za msingi katika halmashauri ya wilaya ya Kilombero unaendelea na utafungwa rasmi ifikapo Machi 3 mwaka huu.
Kwa mujibu wa kaimu afisa elimu msingi katika halmashauri hii, Bi Zakia Fandey amesema kwa hadi kufikia Februari 23 mwaka huu wanafunzi wa darasa la awali walioandikishwa ni 10,879 sawa na asilimia 116 huku waliotazamiwa kuandikishwa walikuwa watoto 9357.
Bi Fandey amesema kuwa wanafunzi waliotazamiwa kuandishwa darasa la kwanza walikuwa 10,962 lakini hadi sasa walioandikishwa ni wanafunzi 11,640 sawa na asilimia 106.
Kwa upande wa mahitaji ya madarasa ya awali,Bi Fandey amesema halmashauri ina mahitaji ya madarasa 333 kwani yaliyopo hivi sasa ni madarasa 46 na upungufu ni madarasa 287 na kwa madarasa ya darasa la kwanza mahitaji ni madarasa 292 na yaliyopo 109 na upungufu madarasa 183.
Kaimu Afisa elimu huyo amesema mafanikio ya zoezi la uandikishaji limeleta changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa kutokana na ongezeko la uandikishaji,upungufu wa madawati kutokana na ongezeko la uandikishaji na upungufu wa walimu wenye ujuzi wa kufundisha madarasa hayo.
Pia changamoto nyingine ni pamoja na jamii za wafugaji kuhama na watoto wao bila kufuata utaratibu na makazi ya wanafunzi kuwa mbali na shule hivyo baadgi ya watoto kutembea mwendo mrefu kufuata huduma.
Hata hivyo kaimu afisa elimu huyo amesema halmashauri imeendelea kutatua changamoto zinazokabili zoezi hili katika maeneo tajwa ikiwemo upungufu wa madawati kwa kutengeneza madawati kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza baada ya hapo itatengeneza madawati kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi ambapo mahitaji ni 1277 na kipaumbele kitazingatia maeneo yaliyoonesha ongezeko kubwa la uandikishaji na zoezi litaanza kwa kutengeneza madawati 422.
Kwa upande wa maboma halmashauri imejidhatiti kupeleka fedha kwa ajili ya kumalizia maboma yote yaliyo tayari kwa kupeleka vifaa vya kiwandani na upande wa walimu serikali inaendelea kuwajengea uwezo walimu wanaofundisha madarasa hayo kwa kuwapatia mafunzo chini ya mradi wa Tusome Pamoja.
Aidha halmashauri inaendelea kuelimisha jamii za kifugaji kuzingatia taratibu za uhamisho kwa watoto wao na pia kuendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii kujitolea nguvu kazi kwa ajili ya ujenzi wa maboma kwa shule mpya ili watoto wasitembee mwendo mrefu kufuata huduma ya elimu.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa