Pichani juu: Mkuu wa wilaya ya Kilombero Ndg James Ihunyo (Aliyeshika kipaza sauti) akiongea na wananchi.
Kutokana na uongozi wa Shamba la mpira namba 165, kata ya Mwaya Wilaya ya Kilombero kuwaruhusu wananchi kufanya shughuli mbalimbali za kilimo na kibinaadamu, imepelekea kuibuka kwa mgogoro mkubwa baina ya Serikali ya wilaya ya Kilombero na wananchi hao, kwa kinachodaiwa kwamba alama za mipaka zilizopandwa na uongozi wa Shamba hilo mwaka 1978 wananchi hawakushirikishwa.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya ya Kilombero Ndg James Ihunyo, Awali shamba hilo lilikuwa ni msitu wa hifadhi ulioanzishwa na wakoloni, na ilipofika 1967 lilitangazwa kama misitu wa kalunga kwa tangazo la serikali la tarehe 08/12/1967, na kupewa namba 350, pia mwaka 1976 msitu huo ulipimwa na wizara ya maliasili na utalii nakupewa JB namba 638, katika mwaka 1980 serikali ilibadilisha matumizi ya msitu huo kutoka kwenye ardhi ya hifadhi na kuwa shamba kwa tangazo la serikali namba 114 la tarehe 01/08/198, na kukabidhiwa General Tyre Ltd, kwa matumizi ya upandaji wa miti ya mpira.
Ndg Ihunyo amesema kuwa zoezi la upimaji na umilikishaji wa shamba hilo, haukuhusisha viongozi wa kijiji vinavyopakana wala wananchi wa vijiji hivyo kama wanavyodai wananchi hao, kwakuwa ardhi hiyo haikuwa ardhi ya kijiji, bali ilikuwa ni ardhi ya hifadhi ambayo ilikuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kumaliza mgogoro huo kwa kufanya jitihada kwa kuwahusisha viongozi wa vijiji vyote vinavyopakana na Shamba hilo kwa nyakati tofauti ili kupata muhafaka wa mgogoro huo, amesema Ndg Ihunyo.
Aidha matokeo ya vikao mbalimbali vilivyokuwa vikifanywa kati ya tarehe 18 na 19 julai 2018 kwa kuwahusisha Maofisa/watumishi wa shamba hilo la mpira, yaliwezesha kufanya uhakiki upya wa shamba hilo,kwa kuwashirikisha baadhi ya wakulima ili kujiridhisha juu ya malalamiko kutoka kwa wananchi.
Ndg Ihunyo aliendelea kusema kuwa, kwa sasa kuna wavamizi wasiopungua 302, na kati ya hao ishirini ni wavamizi wa kilimo na makazi , na 269 wanalima kwa kibali kutoka katika uongozi wa shamba hilo, ambao wanadai maeneo hayo ni ya kwao huku wengi wakiwa na sababu kuwa, maeneo hayo wameyarithi kutoka kwa mababu zao, hivyo kuhalalisha kuwa ni maeneo ya kitu ambacho si kweli, sababu maeneo hayo, walipewa tu kulima ambapo serikali ingekuja kuyachukua muda wowote ule, sababu yalikwishatengwa kwaajili ya kilimo cha mpira na miti.
Sanjari na hayo Ndg Ihunyo amesema kuwa tayari kuna ulinzi mkali sana eneo hilo, na hatakiwi mtu yeyote Yule kufanya shughuli zozote za kimaendeleo eneo hilo, ili kuweza kuepusha migogoro zaidi inayoweza kutokea, sababu maeneo hayo yapo kisheria katika umiliki wa shirika la maendeleo ya taifa (NDC).
Hatahivyo kwa mujibu wa sheria zilizopo, yeyote atakayelima shamba hilo ni mvamizi ,na hii ni kutokana na shamba hilo la mpira kupimwa na kuidhinishwa na Wizara ya ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi, na kumilikishwa (NDC).
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa