Pichani mkuu wa wilaya ya kilombero akiongea na wajumbe hao wa mabaraza ya kata
WIZARA ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Programu ya Kuwezesha Umilikishaji Ardhi{LTSP} imeamua kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa mabaraza ya kata katika utatuzi wa migogoro ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Kilombero.
Mafunzo hayo yatahusu wajumbe wa mabaraza ya kata 26 katika halmashauri hiyo lengo likiwa kuwajengea uwezo wajumbe hao kuhusu utatuzi wa migogoro ya Ardhi kwa mujibu wa sheria na taratibu ili kupunguza mrundikano wa kesi za rufaa kutoka kwenye mabaraza ya kata kwenda baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya.
Mtaalamu Wa Sheria toka LTSP James Balele amesema kitengo cha utekelezaji wa programu ya LTSP katika utekelezaji wa jukumu hilo kilifanya tathmini ya hali halisi ya migogoro ya ardhi katika eneo la programu na tathmini hiyo ilibaini uwepo wa changamoto mbalimbali katika vyombo vya utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Bw Balele ametaja moja ya changamoto hizo ni uwepo wa mrundikano wa kesi katika baraza la ardhi na nyumba la wilaya,uelewa hafifu wa taratibu na sheria za uendeshaji wa baraza la kata na ukosefu wa ujuzi na elimu ya uendeshaji wa mabaraza hayo kwa watendaji husika.
Aidha mafunzo hayo yatawasaidia wajumbe kutambua kazi na wajibu wao ipasavyo katika kutatua migogoro ya ardhi na mafunzo na matumaini yao kuwa mafunzo hayo yataleta tija na ufanisi mkubwa kwa watendaji wa mabaraza ya kata katika utatuzi wa migogoro ya ardhi katika kata nzima,wilaya na mkoa mzima na hii itaimarisha na kuboresha utawala na usimamizi wa ardhi nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti Wa baraza LA Ardhi katika Wilaya za Kilombero,Ulanga na Malinyi Longinus Rugarabamu alisema asilimia 80 ya kesi zinazofika katika baraza lake ni rufaa toka mabaraza ya Ardhi ya kata na kati ya kesi 1400 zinazoendelea katika baraza hilo kesi 800 ni rufaa toka mabaraza hayo.
Ameupongeza mradi Wa LTSP kwa kuandaa mafunzo hayo kwa wajumbe Wa mabaraza ya kata na kusema ana imani baada ya mafunzo hayo wajumbe wataelewa wajibu wao na kutenda haki huku wakipunguza mrundikano Wa kesi katika baraza LA Ardhi LA wilaya.
Akifungua mafunzo hayo,Mkuu wa wilaya ya Kilombero James Ihunyo amechukizwa na utendaji kazi mbovu wa mabaraza ya Ardhi ya kata katika Wilaya hiyo na kuwataka watendaji wabadilike lasivyo serikali itachukua hatua kali ikiwemo kuyafuta.
Bw Ihunyo amesema malalamiko mengi na rufaa zinaonyesha kuwa haki inapindishwa katika mabaraza ya Ardhi ya kata hatimae wananchi kupeleka malalamiko yao katika ofisi yake ama baraza LA Ardhi wilaya ambako wana imani huko ndiko haki inapatikana.
Mkuu huyo Wa Wilaya amewaambia wajumbe hao kuwa wao ndio nguzo muhimu ya serikali katika kutatua migogoro ya Ardhi katika ngazi za kuanzia vijiji hadi kata lakini hali imekuwa tofauti na kuwafanya wananchi kuingia katika gharama kubwa kufuatilia haki hizo wilayani.
Amesema kuwa mabaraza hayo yapo kisheria na ni wajibu kwa wajumbe kutenda haki ili kuondoa misongamano wilayani na kuwaeleza kuwa fursa waliyopata ya mafunzo ni ya mwisho na wapokee vizuri mafunzo na wakiendelea kutokutenda haki atawasiliana na wizara husika ili kufuta mabaraza yote ya Ardhi ya kata wilayani humo.
Programu ya LTSP iliyo chini ya wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi inatekeleza Mpango huo kwa muda Wa miaka mitatu katika Wilaya za Kilombero,Ulanga na Malinyi mkoani Morogoro na moja ya majukumu yake ni kujenga uwezo na kuimarisha taasisi za usimamizi wa ardhi ikiwemo usuluhishi na utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa