Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dokta Kebwe Steven Kebwe, amewataka wananchi wa kijiji cha Kisegese pamoja na vijiji jirani,kusitisha mara moja shughuli za kibinadamu katika msitu wa Namwai uliopo Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro wenye ukubwa wa Hekta 1833.94, ikiwemo ukataji holela wa miti kwaajili ya mbao na uchomaji mkaa,pamoja na kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji ndani ya msitu, kwani wanapaswa kulinda na kuiheshimu mipaka iliyowekwa katika msitu huo.
Agizo hilo amelitoa Novemba,28 mwaka huu, alipotembelea Msitu wa hifadhi wa Namwai uliovamiwa na wananchi wa Kisegese Wilayani humo, kwa kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya msitu huo, ambapo inaweza kupelekea uharibifu wa mazingira utokanao na ukataji miti ovyo, kama vile ukosefu wa mvua pamoja na kupunguza suala zima la Utalii Mkoani Morogoro.
Naye kaimu Afisa misitu wa wilaya ya Kilombero ndugu Magai Pharles Chamba, amesema kuwa walianza utekelezaji wa agizo hilo kwa kufanya shughuli ya kubainisha mipaka ya msitu huo, kwa kuweka alama katika mipaka pamoja na kuweka tuta linalotenganisha eneo la msitu na makazi ya wananchi hao, ambapo wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo walikumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuvamiwa na wananchi kwa lengo la kuzuia zoezi hilo pamoja na kukosekana kwa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa vijiji.
Kwa upande wa baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kisegese, walihoji juu ya uhalali wa msitu huo kwa kusema kuwa kama eneo hilo ni la msitu ilikuwaje wawekezaji na baadhi ya watu kumilikishwa ardhi ndani ya msitu huo, huku wengi wao wakidai kutotambua uhalali wa uwepo wa msitu huo na kuongeza kuwa wao waliliweka eneo la msitu huo katika mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Akijibu hoja hizo za wananchi Kaimu Afisa ardhi na maliasili wilaya ya Kilombero ndugu,Joseph Mgana amesema kuwa, msitu huo upo kisheria na utengwaji wa msitu huo ulianzia katika vijiji vya Mofu na Namwawala na kuongeza kuwa mpango wa matumizi bora ya ardhi wanaouzungumzia wananchi haukusajiliwa hivyo wananchi wanapaswa pia kuzingatia haki za wanyama kwa ujumla.
Hata hivyo Dokta Kebwe ametoa wito kwa Wakuu wa wilaya zote mkoani humo, kutokaa maofisini na badala yake kuwatembelea wananchi ili kubaini changamoto zinazowakabili wananchi,huku akiwataka wananchi hao kuachana na tabia ya uuzaji wa ardhi zao hivyo kupelekea kuvamia maeneo yaliyotengwa kwaajili ya hifadhi.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa