Tarehe 22.08.2024, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mhe. Dunstan Kyobya aliongoza Kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi Wilaya, kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba Itongowa-Mngeta.
Katika kikao hicho mhe. Kyobya ametoa maagizo kadhaa kwa Halmashauri ikiwemo kuhakikisha kasi ya utoaji huduma za chanjo inaongezeka, elimu kuhusu huduma ya usafiri wa dharura kwa wajawazito na watoto wachanga (M-mama) inatolewa kwa wananchi katika maeneo yote ya Halmashauri na wananchi kuhakikisha wanachukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa itokanayo na nyani (Mpox).
Mhe. Kyobya ametumia kikao hicho kutoa maagizo mengine ya jumla ikiwemo Ofisi ya Mkurugenzi kuhakikisha huduma ya umeme inafika mara moja kwenye Vituo vya Afya vya Uchindile na Igima, Zahanati zote zisizo na umeme zifanyiwe utaratibu wa kupelekewa huduma hiyo, miradi ya maendeleo iendelee kusimamiwa ili ikamilike kwa wakati na wananchi waendelee kujiandaa kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Kwa upande mwingine, mhe. Kyobya katika kikao hicho aligawa vitendea kazi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan (gwanda 37 na vishkwambi 35) kwa maafisa ugani 35 kutoka Kata zote za Halmashauri, ikiwa ni sehemu ya kutambua huduma yao kwa jamii na kuendelea kuimarisha mazingira yao ya kazi.
Wataalamu wa afya wa Halmashauri ya Mlimba waliwasilisha mada mbalimbali katika kikao hicho ikiwemo mada za huduma za mama na mtoto, M-mama, homa itokanayo na nyani (Mpox) na huduma za chanjo.
Aidha, kupitia kikao hicho, wananchi wamepaswa kufahamu kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa huduma ya usafiri wa dharura kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga ambao hupata changamoto baada ya kujifungua, ambazo zinaweza kupelekea kifo.
Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Mlimba Dkt. Willy Kopela, huduma ya M-Mama inapatikana kwenye maeneo yote ndani ya Halmashauri kwa kupiga simu namba 115 bure.
Kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi Wilaya hufanyika mara mbili kwa mwaka yaani Januari-Juni na Julai-Desemba na kuhudhuriwa na viongozi wa makundi mbalimbali ikiwemo viongozi wa Dini, Vyama vya Siasa na Wazee.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa