Halmashauri ya Wilaya Mlimba imefanya Mkutano wa Robo ya Pili wa Baraza la Madiwani, kwa lengo la kupokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za Halmashauri kutoka kwa kamati za kudumu za Halmashauri, pamoja na TARURA na RUWASA.
Akiongoza Mkutano huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Mhe. Martha Mkula, amewasisitiza wajumbe kuhamasisha wananchi kulipa ushuru kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato ya halmashauri, ili kuongeza mapato na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya Halmashauri.
Mhe. Mkula pia ameipongeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha Robo ya Pili, huku akiwataka TARURA kuongeza kasi katika ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ili ziweze kupitika kwa wakati wote.
Kupitia mkutano huo, mwakilishi wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilombero, Acrey Lawika, amesema miradi mikubwa ya maji, ikiwemo Mbingu, Igima na Mlimba, imekamilika kwa asilimia 90, na wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Amefafanua kuwa Ofisi ya RUWASA Kilombero tayari imekamilisha mradi wa uchimbaji wa visima vitano, virefu, vya Samia katika vijiji mbalimbali ikiwemo Mkuyuni, Miwangani na Lumumwe, na mpango wa sasa wa Ofisi hiyo ni kuchimba visima vingine vitano katika vijiji vipya ikiwemo Msita na Njage, pamoja na kupanua mradi wa kisima cha Uchindile Lugala.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Kilombero, Mhandisi Fidelis Kessy, ameliambia Baraza la Madiwani kwamba, katika Halmashauri ya Mlimba, madaraja makubwa matatu na barabara zenye jumla ya kilomita 1,060, zinajengwa na kuimarishwa kupitia vyanzo mbalimbali vya fedha kama vile Road Fund, Tozo ya Mafuta, Jimbo la Mlimba na Benki ya Dunia.
Madaraja makubwa yanayojengwa kwa fedha za Benki ya Dunia ni daraja la Mbasa katika kata ya Mchombe, Isago katika kata ya Mngeta na Matete katika kata ya Mbingu.
Aidha, TARURA inaendelea na ujenzi wa barabara za changarawe na lami, pamoja na makaravati na madaraja katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ili kuhakikisha barabara zinapitika kwa wakati wote.
Baraza la Madiwani limepongeza juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha huduma kwa jamii, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara na upelekaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Mkutano huo umehudhuriwa na Waheshimiwa Madiwani kutoka kata 16 za Halmashauri, viongozi wa vyama vya siasa ikiwemo Katibu wa Chama cha Mapinduzi, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero pamoja na Kamati ya Usalama ya Wilaya.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa