Halmashauri ya Wilaya Mlimba inaendelea kupokea waajiriwa 118 wa kada mbalimbali, waliopangiwa ajira na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kibali cha mwaka wa fedha 2025/2026.
Ajira hizo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kutoa ajira 12,000 ndani ya siku 100 za uongozi wake, ambapo hadi sasa ni takribani siku 81 tangu kuapishwa kwake Novemba 01, 2025.
Utoaji wa ajira hizo unalenga kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kupunguza uhaba wa watumishi katika sekta mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba amesema kuwa kupokelewa kwa waajiriwa hao ni hatua muhimu katika kuimarisha rasilimali watu, hususan katika sekta zinazogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.
Ameeleza kuwa Halmashauri imejipanga kuhakikisha waajiriwa hao wanapangiwa maeneo ya kazi kulingana na mahitaji halisi, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kufanikisha malengo ya maendeleo ya halmashauri.
Miongoni mwa waajiriwa hao ni watumishi wa sekta ya afya wakiwemo madaktari, wauguzi na wahudumu wa afya ngazi ya jamii. Kada nyingine ni pamoja na kilimo, ujenzi, mawasiliano na elimu.
Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba inaishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuipatia ajira hizo, ambazo zinatarajiwa kusaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa halmashauri hiyo.
Kwa upande wao, waajiriwa hao wameishukuru Serikali kwa fursa ya ajira waliyoipata, huku wakiahidi kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na kujituma mara watakapoanza rasmi utumishi wao.
Waajiriwa hao wameanza kupokelewa Jumatatu tarehe 19.01.2026.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa