Mradi wa Mifumo ya Chakula, Matumizi ya Ardhi na Urejeshaji wa Uoto wa Asili (FOLUR) umeingia rasmi hatua ya utekelezaji kwa vitendo, baada ya Sekretarieti ya mradi huo kukutana Man’gula–Ifakara Januari 15–17, 2026, kwa lengo la kuunganisha mipango ya usimamizi wa shughuli za kisekta za kilimo, ardhi, misitu, wanyamapori na maji, ili kuwa na mpango jumuishi wa utekelezaji wa shughuli za mradi katika maeneo ya mradi ambayo ni Halmashauri ya Wilaya Mlimba na Halmashauri za Kaskazini A na B-Unguja.
Hatua hiyo inaashiria kuanza kwa mwaka wa pili wa utekelezaji wa Mradi wa FOLUR Tanzania, unaofadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Uhifadhi wa Mazingira (GEF), na kutekelezwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mratibu wa Mradi katika Halmashauri ya Wilaya Mlimba, Ndg. Joseph Mgana, alisema kuwa hatua ya kuanza utekelezaji wa vitendo imefikiwa baada ya kukamilika kwa maandalizi yote ya awali ya mradi.
Alisema maandalizi hayo yalijumuisha kuanzishwa kwa ofisi ya mradi, kuutambulisha mradi kwa menejimenti za halmashauri husika, pamoja na kwa wananchi wa vijiji vinavyotarajiwa kunufaika na mradi kote Tanzania Bara na Zanzibar.
“Katika mwaka wa kwanza wa mradi, tumepokea na kujadili matokeo ya tafiti za kisekta kutoka kwa wadau wa serikali na binafsi, wakiwemo washauri elekezi na watekelezaji wenza. Matokeo hayo yametumika kuandaa mipango kazi ya kisekta, ambayo sasa tunaenda kuitekeleza kwa pamoja,” alisema Ndg. Mgana.
Aliongeza kuwa baada ya kukamilika kwa hatua hiyo ya maandalizi, mradi sasa unaanza utekelezaji jumuishi katika vijiji vyote 49 vya mradi vilivyopo Tanzania Bara na Zanzibar.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa FOLUR kutoka Wizara Simamizi ya Mradi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Ndg. Wanjala Mgaywa, alisema kuwa FOLUR ni mradi wa kwanza wa kitaifa unaolenga kuimarisha uhifadhi wa rasilimali maji, ardhi na misitu kwa mtazamo wa pamoja, huku kilimo endelevu cha zao la mpunga kikiwa ni eneo mahsusi la utekelezaji.
“Tunaamini kuwa ili mpunga ulimwe kwa tija na kwa uendelevu, ni lazima tuhifadhi misitu ambayo ndiyo chanzo kikuu cha maji. Aidha, ni muhimu kuweka utaratibu wa matumizi bora ya maji, pamoja na kupanga matumizi ya ardhi ili mkulima alime katika eneo dogo lakini azalishe kwa wingi,” alisema Ndg. Mgaywa.
Alifafanua kuwa kupitia mradi wa FOLUR, wakulima watasaidiwa kupanga na kutumia ardhi yao kwa tija, huku juhudi za uhifadhi wa misitu zikichangia uzalishaji wa hewa ya kaboni itakayokuwa na manufaa ya kiuchumi kwa halmashauri za mradi na taifa kwa ujumla.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, jumla ya vijiji 23 kutoka kata za Mngeta, Mchombe, Mofu, Chin’anda, na Chisano vinatarajiwa kunufaika na mradi wa FOLUR. Vijiji hivyo ni Mofu, Kalenga, Ikwambi, Ihenga, Miyomboni, Mkusi, Njage, Mchombe, Nakaguru, Ijia na Lukolongo.
Vingine ni Mngeta, Kidete, Isago, Mkangawalo,Luvilikila, Ikule, Itongowa, Chin’ganda, Lufulu, Udagaji, Chisano na Mgugwe.
Mradi wa FOLUR unalenga kuchangia katika kuimarisha mifumo endelevu ya uzalishaji wa chakula, kuhifadhi rasilimali asilia na kuboresha maisha ya wananchi katika maeneo ya mradi kupitia mbinu jumuishi za usimamizi wa ardhi na mazingira.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa