Halmashauri ya Wilaya Mlimba imeazimia kuhimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata milo miwili shuleni, ikiwa ni pamoja na uji wenye virutubisho wakati wa asubuhi na chakula cha mchana kinachozingatia mlo kamili.
Vilevile, halmashauri imeazimia kutoa elimu ya virutubisho kwa wakuu wa shule ili waweze kuhimiza wanafunzi kunywa uji na ugali wenye virutubisho na kuacha mazoea ya kula wali pekee.
Maazimio hayo yamekuja baada ya wasilisho la taarifa ya utekelezaji wa Afua za Lishe, lililofanywa na Afisa Lishe wa Halmashauri, Ndg. Bodygadi Buhari, katika Kikao cha Tathmini ya Lishe kwa Kipindi cha Julai–Desemba, kilichofanyika Jumamosi tarehe 17 Januari 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri, kikiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mlimba, Mhe. Martha Mkula, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Wakili Dunstan Kyobya.
Kupitia taarifa hiyo, wajumbe walipongeza juhudi za Halmashauri kununua mashine tano za kuongeza virutubisho kwenye unga wa mahindi, ambazo tayari zimesambazwa katika kata tano zenye wamiliki wa mashine hizo. Wajumbe walisema mashine hizo zitasaidia kuimarisha Lishe bora kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Pia, wajumbe walihimiza usimamizi makini wa vyakula shuleni ili kuhakikisha vinajumuisha makundi yote saba ya chakula na kuimarisha afya ya mwili na akili za wanafunzi.
Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Martha Mkula amewataka wazazi na walezi kuelewa kwamba kuchangia chakula cha mtoto shuleni si hiari bali ni wajibu, huku akisisitiza kuwa mahindi ni lazima yawepo ili kusaidia upatikanaji wa uji na ugali wenye virutubisho.
Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Lishe Buhari, utekelezaji wa Afua za Lishe katika Halmashauri ya Mlimba unafanyika kwa mafanikio makubwa, kwani hakuna alama nyekundu zilizorekodiwa katika afua zote za lishe kwa wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, na upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Katika kikao hicho, Mratibu wa Huduma za Bima wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba, Dkt. Amani Nkilingi, pia aliwajengea uelewa wajumbe kuhusu Bima ya Afya kwa Wote, ambapo alisema kuwa mpango huo ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita, ukiendana na Dira ya Taifa 2050, Malengo Endelevu ya Milenia 2030, na Ilani ya CCM 2025–2030.
Dkt. Nkilingi alifafanua kuwa lengo ni kuondoa matabaka kwenye matibabu na kwamba Serikali itagharamia bima kwa makundi maalumu ambayo ni wazee, watoto, wajawazito na wenye ulemavu.
Aidha, wananchi wengine watajiunga kwa hiari kwa gharama ya Sh. 150,000 kwa kaya isiyozidi watu sita, ambapo jumla ya huduma 372 zitatolewa ikiwemo huduma za kibingwa, uchunguzi, maabara, radiolojia, dawa na vifaa tiba. Aidha, bima ya Afya kwa Wote haitasababisha kuachishwa kwa bima nyingine kama NHIF, isipokuwa Bima ya CHIF tu itasimamishwa pale itakapokoma muda wake.
Kikao cha Tathmini ya Lishe kwa Kipindi cha Julai-Desemba cha Halmashauri ya Mlimba kilihudhuriwa na wadau mbalimbali, ikiwemo Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba, watendaji wa kata, na wakuu wa idara na vitengo vya Halmashauri.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa