Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba imeanza maandalizi ya zoezi la ugawaji bure wa vyandarua vyenye dawa kwa kaya zake zote, kufuatia ujio wa wataalamu kutoka Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, waliowasili halmashaurini hapo tarehe 16 Januari, 2026 kwa lengo la kutambulisha mpango huo wa Serikali.
Akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Madiwani la upokeaji wa Taarifa ya Utekelezaji wa Shughuli za Halmashauri kwa Kipindi cha Robo ya Pili (Oktoba–Desemba), uliofanyika tarehe 17 Januari, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dkt. Christina Guveti, amesema kuwa jumla ya vyandarua 174,769 vinatarajiwa kusambazwa kwa wananchi wa halmashauri hiyo.
Dkt. Guveti amesema kuwa ugawaji huo utafanyika kwa utaratibu wa chandarua kimoja kwa kila wanakaya wawili, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kudhibiti na kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria.
Ametoa wito kwa Waheshimiwa Madiwani kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la utambuzi wa kaya, litakalofanyika kwa muda wa majuma mawili kuanzia Jumatatu tarehe 19 Januari, 2026, katika kaya zote, kambi za jeshi pamoja na shule za sekondari zilizopo ndani ya halmashauri.
Aidha, amewataka Watendaji wa Kata na Vijiji kusimamia zoezi hilo kwa haki na uwazi, ili kuhakikisha kaya zote zinanufaika na ugawaji wa vyandarua hivyo, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha huduma muhimu za afya zinawafikia wananchi wote.
Dkt. Guveti ameongeza kuwa zoezi la ugawaji wa vyandarua vyenye dawa linasimamiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), baada ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia sekta ya afya kufanya utafiti uliobaini kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba ni miongoni mwa halmashauri saba kati ya tisa za Mkoa wa Morogoro zenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria.
Amefafanua kuwa, kutokana na jiografia ya Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, vyandarua hivyo vitasambazwa katika vitongoji vyote ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma hiyo kwa usawa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Mhe. Martha Mkula, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha zoezi la ugawaji wa vyandarua hivyo, sambamba na utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya vyandarua, hatua itakayochangia kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria halmashaurini humo.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa