HALMASHAURI YA WILAYA YA KILOMBERO KUJIPANGA KUANDAA MAONESHO YA NDANI YA WAKULIMA
Katika kuhakikisha wakulima wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero wanapata fursa ya kuonesha bidhaa zao za kilimo pamoja na kujifunza mbinu za kisasa za kilimo ili kuongeza pato lao, halmashauri ya wilaya ya wilaya hiyo inajipanga ili kuhakikisha kunakuwa na maonesho ya ndani ya bidhaa za kilimo katika halmashauri hiyo.
Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Kilombero Mheshimiwa James Ihunyo alipotembelea banda la halmashauri hiyo katika maonesho ya 25, ya nanenane kwa Kanda ya Mashariki yaliyofanyika katika viwanja vya Mwl.Julius Kambarage Nyerere katika Manispaa ya Morogoro Agosti ,8 ya mwaka huu.
‘‘Tuna taasisi zetu za kilimo kama Katrini pamoja na skimu mbalimbali za kilimo cha umwagiliaji na pia tumekuwa tukiwasisitiza maafisa ugani kuwatembelea wakulima wetu wote ili kuwaelimisha juu ya kilimo cha kisasa na matumizi bora ya pembejeo za kilimo na pia tangu tulipoteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumezunguka sana ndani ya halmashauri ya wilaya ya Kilombero tukisisitiza juu ya kilimo bora, sasa nadhani ni wakati muafaka wa kuandaa maonesho ya ndani yatakayoleta chachu kwa wakulima wa Kilombero’’ alisema mheshimiwa Ihunyo.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Mlimba Mheshimiwa Suzan Kiwanga alisema kuwa tangu alipoanza kuhudhuria maonesho mbalimbali ya nanenane kwa miaka tofauti tofauti, ameshuhudia mabadiliko mbalimbali kwa maonesho ya mwaka huu ikiwemo ubunifu wa zana za kisasa za kilimo kutoka kwa Watanzania wazalendo ikiwa ni pamoja na waliotoka wilayani Kilombero ambapo aliongeza kuwa atashirikiana na halmashauri ya wilaya ya Kilombero ili kuandaa utaratibu wa kuandaa maonesho ya ndani ya kilimo yatakayoanzia katika ngazi ya tarafa au jimbo badala ya kusubiri maonesho ya nane nane pekee.
Mheshimiwa Kiwanga alitumia fursa hiyo pia kutoa wito kwa vikundi mbalimbali kutoka katika jimbo la Mlimba wilayani Kilombero kujiandaa vyema ili kuhakikisha kwamba wanashiriki katika maonesho ya mwaka 2018,ili kuweza kujitangaza pamoja na kutangaza bidhaa mbalimbali wanazozalisha katika vikundi vyao.
‘‘Wito wangu kwa wananchi wa Mlimba wasijione wanyonge na ni vema wakajiandaa mapema hususani vikundi vilivyopata fedha kutoka halmashauri (Kilombero) kujitokeza ili kushiriki katika maonesho yajayo ili kutangaza bidhaa zao pamoja na kujifunza kutoka katika vikundi vingine vitakavyoshiriki katika maonesho hayo’’
Katika maonesho hayo yaliyohusisha wilaya zote na halmashauri za miji kutoka katika mikoa yote inayounda Kanda ya Mashariki ambayo ni pamoja na Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Morogoro, wilaya ya Kilombero iliweza kuonesha bidhaa mbalimbali za kilimo ikiwa ni pamoja na ufugaji wa kuku kisasa ambapo mtaalamu wa ufugaji wa kuku kutoka wilayani humo bwana Emmanuel Tilya alitambulisha teknolojia rahisi ya utotoleshaji na utunzaji wa vifaranga vya kuku chotara wenye mchanganyiko wa mbegu kutoka Tanzania na Malawi kwa kutumia vyungu ambapo pia alielezea umuhimu wa kuwakata kuku midomo njia aliyosema kuwa husaidia kupambana na tabia mbaya za kuku ikiwemo unywaji wa mayai na kudonoana huku akitoa wito kwa wafugaji wa kuku kuacha kufuga kwa mazoea na kuhamia kwenye ufugaji wa kisasa wenye tija ili kuweza kujipatia faida kubwa.
Kwa upande wa ufugaji wa nyuki, Halmashauri ya wilaya ya Kilombero iliwakilishwa na wafugaji kutoka katika Tarafa ya Mang’ula waliokuwa na mizinga ya asili na rafiki kwa mazingira inayotumika katika ufugaji wa nyuki wadogo ambayo walieleza kuwa huwavutia nyuki kwa wingi kutokana na uasili wake ambao hufanana na mapango.
‘‘Sisi tunashirikiana na watu wa mazingira katika ufugaji wetu na hivyo mizinga yetu ni rafiki kwa mazingira na pia hutumika katika nyakati zote iwe ni masika au kiangazi na pia inadumu kwa muda mrefu’ alisema Bi.Zufinala Kuluka mwakilishi wa kikundi cha wafugaji hao wa nyuki kutoka katika tarafa ya Mang’ula wilayani Kilombero’
Aidha kwa upande wa zao la mpunga halmashauri ya wilaya ya Kilombero ilitambulisha mashine mpya ya kisasa yenye uwezo wa kufanya kazi tatu kwa wakati mmoja ambazo ni pamoja na kuchimba mashimo kuweka mbegu pamoja na kufukia ambapo pia wajasiriamali mbalimbali kutoka wilayani humo waliweza kuuza mchele wenye viwango bora unaolimwa katika halmashauri hiyo.
Halmashauri ya Kilombero pia iliweza kuonesha zao la kokoa lenye thamani kubwa sokoni kwa sasa ambapo kampuni ya Kokoa Kamili inayofanya shughuli zake wilayani humo kupitia mwakilishi wake Bi, Sabina ilieleza kuwa kupitia maonesho hayo, kokoa kutoka katika kampuni yao imefanya vizuri katika soko hali aliyoelezea kwamba imetokana na ukweli kwamba wamekuwa wakipata kokoa bora kutoka wilayani Kilombero tofauti na maeneo mengine.
Katika hatua nyingine baadhi ya wananchi waliotembelea banda la halmashauri ya wilaya ya Kilombero katika maonesho hayo wameipongeza halmashauri hiyo huku wengi wakielezea kufurahishwa zaidi na teknolojia ya ufugaji wa kuku hususani madawa mbalimbali ya asili ya kuku pamoja na mabanda ya kisasa ya kufugia huku baadhi yao wakiongozana na watoto pamoja na wajukuu zao kwa lengo la kuwapatia fursa ya kujifunza mambo mbalimbali katika banda hilo.
Maonesho ya nanenane kwa kanda ya Mashariki kwa mwaka 2017 ni maeonesho ya 25 yaliyojumuisha wilaya za mikoa yote inayounda kanda hiyo ambapo kwa upande wa halamashauri ya wilaya ya Kilombero iliweza kuwakilishwa na idara malimbali kutoka katika halmashauri hiyo ikiwemo kilimo na ufugaji , vikundi mbalimbali vya wafugaji, wakulima, vikundi vya ushonaji nguo , wajasiriamali wadogo wanaojihusisha na utengenezaji wa bidhaa za ngozi na shanga huku yakiwa na kaulimbiu isemayo, zalisha kwa tija mazao na bidhaa za kilimo, mifugo pamoja na uvuvi ili kufikia uchumi wa kati.
Imeandikwa na Ibrahim Rojala
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa