HALMASHAURI ya wilaya ya Mlimba inakadiria kupata jumla ya shilingi bilioni 33,805,381,339.19 kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Hayo yamebainishwa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Mhandisi Stephano Kaliwa wakati wa mkutano maalum wa bajeti wa baraza la madiwani uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita makao makuu ya halmashauri hiyo Mngeta.
Mhandisi Kaliwa amesema bajeti hiyo imezingatia maeneo mahsusi na ya kipaumbele yaliyoainishwa katika mpango mkakati wa halmashauri wa mwaka 2016/2017-2021/2022,mwongozo wa uandaaji wa bajeti wa mwaka wa fedha wa 2021/2022 na mpango wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano 2016/2017-2020/2021(FYDP II).
“Maeneo mengine yaliyozingatiwa katika bajeti ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa Ccm ya mwaka 2020/2025,sheria ya bajeti sura 439 pamoja na kanuni zake,mkakati wa taifa dhidi ya rushwa awamu ya tatu,malengo endelevu ya maendeleo na mwongozo wa ushirikiano wa kimaendeleo,”alisema.
Mkurugenzi huyo mtendaji ameyataja maeneo yaliyopewa kipaumbele katika sekta ya kilimo kuwa ni ununuzi wa mbegu za korosho kilogramu 1000 na kuandaa maandiko ya miradi ya umwagiliaji Udagaji na Kisegese na upande upande wa mifugo ni kutoa huduma ya chanjo mbalimbali kwa mifugo sambamba na kuboresha huduma ya uogeshaji kwa kujenga josho moja katika kijiji cha Namwawala.
Ameyataja maeneo mengine yaliyopewa kipaumbele ni katika sekta ya elimu ya msingi na sekondari kwa ukamilishaji wa maboma ya madarasa na nyumba za walimu,kuwapa kipaumbele walimu wanaoishi shule za pembezoni na kukagua ubora wa elimu mara kwa mara katika shule za serikali na binafsi.
“Kwa upande wa sekta ya Afya tumepanga kuendeleza ujenzi wa kituo cha Afya Chita na kuanza ujenzi wa kituo cha Afya Igima na upande wa maji tumepanga kuboresha huduma za maji katika taasisi za umma kama shule na vituo vya afya kwenye shule za msingi 52,sekondari 10 na vituo vya afya 21”alisema.
Mhandisi Kaliwa amesema pia wanataraji kuboresha ukusanyaji wa mapato ya halmashauri ili kufikia malengo ya makusanyo kwa kutumia sheria ndogo na usimamizi mzuri wa matumizi na kutoa mikopo kiasi cha shilingi milioni 275 kwa wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.
Akielezea ukusanya wa mapato ya ndani,Mhandisi Kaliwa amesema jumla ya shilingi bilioni 2,750,000,000 wanakadiria kukusanya kutoka vyanzo vyake vya ndani kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
“Makadiro ya mapato hayo yanalengwa kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwemo ushuru wa mchele na mazao mengine,ushuru wa nyumba za kulala wageni,ushuru wa huduma,ushuru wa kuzoa taka,ukodishaji wa mali za halmashauri,ada ya kuuza kiwanja na leseni za biashara,”alibainisha.
Vyanzo vingine ni pamoja na vibali vya burudani,ushuru wa mazao ya misitu,ushuru wa vibanda vya soko,huduma za ardhi,ada za mifugo,ushuru wa machinjio,ushuru wa samaki,leseni za uvuvi,ada za leseni za vyombo vya uvuvi na faini mbalimbali.
Hata hivyo mkurugenzi huyo amesema kuwa halmashauri hiyo imejiwekea mradi wa kimkakati ili kuongeza mapato ya halmashauri ambapo wamepanga kujenga skimu ya umwagiliaji Katina bonde la Kisegese ili kuboresha kilimo ambapo shilingi bilioni 13,195,356,140 zitatumika.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri hiyo Innocent Mwangaza amesema bajeti hiyo inalenga kumsaidia mwananchi wa jimbo la Mlimba ambapo wameamua kuongeza vyanzo vipya vya mapato ikiwemo kukodisha majengo yao yaliyopo Ifakara na Mlimba na pia katika kujali afya za wananchi wameamua kuweka maduka ya madawa katika vituo vya Afya Mlimba na Lukolongo.
“Bajeti hii itamkomboa mwana Mlimba na msukumo wetu kama madiwani ni kuhakikisha mapato tunaweka mipango ya kuongeza mapato ikiwemo kukodisha majengo yetu tuliyoyaacha pale Ifakara na jengo la benki pale Mlimba na tumepanga kuyafikia maeneo yote wanayoishi wafugaji ili kujua wapo wangapi na mifugo ipo mingapi lengo ni kuwa na mifugo michache na kupata mapato halali,”alisema.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa