ZAIDI ya kaya 10 katika kata ya Uchindile wilayani Kilombero zimekosa makazi baada ya nyumba zao kuteketea kwa moto na ekari zaidi ya 6000 za miti kuungua na hadi sasa chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.
Tukio hilo limetokea wiki iliyopita katika vijiji vya Uchindile na Lugala kata ya Uchindile ambayo asili yake imezungukwa na mashamba makubwa ya miti ya kutengeneza nguzo na karatasi ambapo moto huo ulianzia katika mashamba hayo kisha kuenea katika mashamba ya wananchi na kuwasababishia athari kubwa ya mali zao.
Afisa mtendaji wa kata hiyo Joachim Limbela alisema moto huo ulianza majira ya mchana na kutokea kaskazini mashariki ya kijiji cha Uchindile na uliwaka kwa muda wa siku saba na kuteketeza nyumba hizo kumi na mashamba ekari za mashamba zaidi ya 6000 za wananchi.
Limbela alisema baada ya siku tatu moto mwingine uliwaka katika mashamba ya wananchi katika kijiji cha Lugala na kuteketeza ekari zaidi ya 400 na kutaja athari walizopata wananchi kuwa ni kuunguliwa kwa nyumba zao na vifaa vya ndani sambamba na mifugo yao na hadi sasa chanzo cha moto huo hakijajulikana.
Daniel Isonga ambaye ni mmoja wa walioathirika na moto huo alisema kuwa moto ulianza majira ya saa 8 mchana yeye akiwa nyumbani na kuanza kutoa vifaa vya ndani lakini moto ulivyozidi alishindwa kuokoa baadhi ya vitu ambavyo viliteketea kwa moto na kusema kuwa zaidi ya ekari zake 60 za miti ziliteketea na pia kaya zake 4 zimeathirika na janga hilo.
Naye Angelina Kyunga alisema yeye ameunguliwa ekari zake 10 za miti pamoja na mifugio kama kuku na ng’ombe na moto huo umemtia umaskini na kuiomba serikali kumsaidia.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero Dennis Londo alisema familia 10 nyumba zao zimeteketea na kaya zaidi ya 100 zimeathirika na moto huo na hata wawekezaji wa kampuni ya Green resource ambao wanamiliki mashamba makubwa katika kata hiyo wameathirika kwa kiasi kikubwa kwa kuteketea mashamba yao.
Londo aliipongeza ofisi ya mkuu wa wilaya ya Mufindi kwa kusaidia kutoa huduma za haraka tokana na ukaribu uliopo baina ya kata na wilaya hiyo ambapo walifanikiwa kuzima moto kwa kushirikiana na wanmanchi na kusema kuwa uongozi wa mkoa wa Morogoro umeagiza kufanyika kwa tathmini ili kuweza kupata idadi ya hasara iliyopatikana kisha kuweza kuwasaidia waathirika.
Hata hivyo halmashauri hiyo imeweza kutoa misaada michache kwa waathirika ikiwemo mafuta ya kula,sukari na mchele na zoezi hilo lilifanyika punde janga lilipotokea ambapo mwenyekiti wa halmashauri alitoa vifaa hivyo na kisha nae mkurugenzi huyo alitoa msaada kwa familia zilizounguliwa nyumba zao ili waweze kurudi katika hali yao ya kawaida.
Kutokana na jiografia ya kata ya Uchindile kuwa ni ngumu kufikika ilibidi kikosi cha jeshi la kujenga taifa Mafinga mkoani Iringa kwenda kutoa msaada wa uzimaji wa moto ambao uliwaka kwa siku saba mfululizo
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa