Tarehe 08.07.2024 Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Wilaya Mlimba, imetembelea na kukagua miradi ya maendeleo iliyo tekelezwa, inayotekelezwa na inayo tazamiwa kutekelezwa na Halmasahuri kwenye Kata mbalimbali ikiwemo Kata ya Masagati
Ikiwa katika Kata ya Masagati, Kamati ilitembelea shule ya msingi Lwamate na kuridhia kuimarisha miundombinu ya shule hiyo kwa kukamilisha jengo la nyumba ya walimu, vyumba vitatu vya madarasa na Ofisi ya walimu ili kuweza kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji shuleni hapo.
Sambamba na hilo, Halmashauri kwenye bajeti yake ya mwaka huu wa fedha imetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa madawati shuleni hapo.
Wakati Kamati ya Fedha inawasili shuleni hapo, ilikuwa jioni na wanafunzi wengine walikuwa wamekwisha kurudi nyumbani. Wanafunzi sita tu, wa darasa la saba ndio walio kuwa wamesalia shuleni hapo wakijisomea chini ya usimamizi wa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ndugu Godwin Sing’onje.
Ni jambo linalo gusa moyo sana kuona jinsi elimu inavyotafutwa kwa bidii, kwani jumla ya wanafunzi wa darasa la saba waliopo shuleni hapo ni nane tu, na jioni hiyo wawili kati yao hawakuwa wamehudhuria shule kwa sababu za kiafya, lakini kwa pamoja hao ndio wanao unda darasa la saba shuleni Lwamate.
Inavutia kuona Mwalimu Mkuu kwa kushirikiana na walimu wenzake wanne, wa shule hiyo wanavyo simamia taaluma na maelekezo ya Serikali kwani pamoja na kuwa shule hiyo iko pembezoni, watoto wote 137 wa darasa la kwanza hadi la saba, wanapata huduma ya chakula wawapo shuleni.
Kamati ya fedha ilijionea magunia matatu ya mahindi kwa ajili ya chakula cha wanafunzi, yakiwa yamehifadhiwa kwenye mojawapo ya vyumba vilivyopo shuleni hapo.
Lakini hata ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba kwenye mtihani wa Taifa ni wa daraja C na wamekuwepo wanafunzi ambao wamekuwa wakichaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari, hasa kwenye Shule ya Sekondari ya Kata hiyo, ijulikanayo kwa jina la Masagati.
Mwaka 2022, wanafunzi 19 shuleni Lwamate walifanya mtihani wa darasa la saba, ufaulu wa shule ulikuwa daraja C, na 14 kati yao walipangwa kujiunga na kidato cha kwanza shule ya sekondari Masagati.
Mwaka 2023, wanafunzi 12 walifanya mtihani wa Taifa wa darasa la saba, ufaulu wa shuleulikuwa daraja C tena, na wanafunzi 08 walipangwa kujiunga na kidato cha kwanza shuleni Masagati.
Mwaka huu, 2024 wanafunzi 08 wanatazamiwa kufanya mtihani wa Taifa wa darasa la saba na pasina shaka matokeo yao huenda yakawa mazuri zaidi kwa sababu Halmashauri imejizatiti kuboresha mazingira ya ujifunzaji na undishaji ya shuleni hapo.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ndugu Godwin Sin’gonje amesema uhaba wa maji, stoo ya chakula, choo cha walimu, ofisi na nyumba za walimu ndio changamoto kubwa zinazo ikabili shule ya Lwamate, na endapo zitatatuliwa bila shaka hata ufaulu wa wanafunzi utaimarika zaidi.
Pamoja na kuwa Kata ya Masagati ipo umbali wa takriban kilomita 160 kutoka lililpo Jengo la Utawala la Halmashauri - Mngeta, bado wananchi wake wanaendelea kupata huduma wanazo stahili kutoka Halmashauri.
Ipo Zahanati, shule ya kutwa ya sekondari lakini ina hosteli kwa ajili ya wanafunzi wa kike na hivi karibuni Halmashauri inataraji kuanza kujenga Kituo cha Afya kwenye Kata hiyo ili kuimarisha zaidi huduma za afya kwa wananchi wa Masagati.
Kamati ya Fedha ilifanikiwa kutembelea eneo pendekezwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiko cha afya.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa