Na; Milka Kaswamila- Afisa Habari Mlimba DC
Kamati ya Kudhibiti na Kukagua Shughuli za Serikali ( LAAC), tarehe 25.03.2025 imefanya ziara kwenye Halmashauri ya Wilaya Mlimba kukagua Mradi wa Ujenzi wa Nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji na Mradi wa Ujenzi wa Wodi Tatu na jengo la kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya, ya Halmashauri hiyo.
Ziara hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Halima Mdee ambapo awali walipokea taarifa ya miradi yote mitatu kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ndg. Jamary Idrisa Abdul kisha wakauliza maswali na kuagiza Ofisi ya Mkurugenzi kuhakikisha Halmashauri inaendelea kufuata taratibu zote za upatikanaji wa vibali vya ujenzi wa miradi kutoka mamlaka za juu ikiwemo Ofisi ya Rais TAMISEMI na kutoa taarifa katika mamlaka zote husika endapo Halmashauri itafanya mabadiliko ya matumizi ya fedha za miradi.
Hata hivyo, kamati ya LAAC kupitia mwenyekiti wake, Mhe. Halima Mdee wamesema wameridhishwa na miradi waliyoikagua na wamempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo pamoja na timu yake ya wataalamu kwa usimamizi mzuri wakisema thamani ya fedha iliyo tumika imeendana na ubora wa majengo husika.
Kwa upande wake Naibu Waziri kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Festo Dugange amesema amependezwa kuona watumushi wa Halmashauri wakiwa na afya njema na miradi yao ikiwa ni mizuri.
“Tumeona nyumba ya Mkurugenzi nzuri sana, wodi za wagonjwa nzuri sana, Wakuu wa Idara ni wengi, watumishi wamenawiri, na zaidi tumefurahi kuona mmeitumia vizuri nyongeza ya milioni 250 mliyoletewa na Ofisi ya TAMISEMI ili kukamilisha ujenzi wa zile wodi tatu. Hongereni sana”. Alisema Mhe. Dugange.
Kwa mujibu wa taarifa iliyo wasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji, Ndg. Jamary Idrisa Abdul, ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi umegharimu kiasi cha shilingi milioni 335.65 na wodi tatu na jengo la kuhifadhia maiti zimegharimu jumla ya shilingi milioni 971.37.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Wakili Dunstan Kyobya aliishukuru LAAC na kuahidi kuhakikisha anasimamia utekelezwaji makini wa maagizo yote iliyo yatoa kwa Halmashauri ya Mlimba. Aidha, alitumia wasaa huo kueleza mazuri ya Mlimba na kuwaalika wajumbe wa kamati kuwa mabalozi wa Mlimba kule waendako na wao kuja kuwekeza hasa katika sekta ya kilimo ambapo Halmashauri kwa sasa zao lake kubwa la biashara ni mchele, na mengine ni ufuta, kokoa, mbaazi, korosho na chikichi.
Hii ilikuwa ni ziara muhimu katika kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inasimamiwa vyema na inawafaidisha wananchi wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba.
Kamati ya LAAC inaendelea na kazi yake ya kudhibiti na kukagua shughuli za serikali ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Serikali za Mitaa unafanyika kwa usahihi na kwa manufaa ya umma.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa