MKUU wa wilaya ya Kilombero Hanji Godigodi ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Mlimba kuhakikisha kuwa inamaliza ujenzi wa vyumba vya madarasa 78 kabla ya Disemba 10 mwaka huu ili kujiandaa kuwapokea wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwakani.
Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika jana Mngeta wilayani humo,Godigodi amesema licha ya kukamilika kwa madarasa hayo pia yanatakiwa kukamilika madarasa shikizi mawili,nyumba moja ya mtumishi mtumishi na bweni moja la watoto.
Godigodi amesema halmashauri hiyo imepokea kiasi cha shilingi bilioni 1,680,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 78,bweni moja la watoto,nyumba moja ya mtumishi na madarasa mawili shikizi.
Amesema fedha hizo zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuona wanafunzoi wote wanakaa madarasani na pia kuepusha wanafunzi hao na msongamano ambao unaweza kusababisha maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
Amebainisha kuwa licha ya kuwaepusha wanafunzi na ugonjwa wa Corona pia amewapunguzia wananchi katika uchangiaji wa ujenzi wa madarasa hivyo kuwataka wahusika kutumia vizuri fedha hizo na kutoa rai kuwa fedha hizo ni za moto na ataezichezea zitaondoka nae.
Mkuu huyo wa wilaya amesema kwa juhudi za watendaji wa halmashauri na madiwani ana uhakika wanafunzi wote waliofaulu wataingia darasani hapo Januari mwakani.
Amesema fedha zimeshaingia katika akaunti za shule hivyo kuiagiza menejimenti kuhakikisha kuwa kila diwani aliyepata fedha katika shule yake kujulishwa mapema ili nae aweze kuwajulisha wananchi wake anaowaongoza wafahamu fedha hizo zimetoka wapi.
Amewataka madiwani kusimamia fedha hizo ili kupata thamani ya fedha kwa ujenzi wa madarasa imara na madhubuti na wasiwaingilie mafundi katika kazi zao za utendaji.
Aidha mkuu huyo wa wilaya amewataka madiwani hao kuhamasisha wananchi wakapate chanjo ya Covid 19 kwani ni salama huku pia akiagiza wananchi wahimizwe na kwenda kwa watendaji kuchukua vitambulisho vyao vya uraia.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mlimba Innocent Mwangasa ameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu kwa kuwapatia fedha hizo na kusema kuwa zimefika kwa wakati na kuahidi kuwa watatekeleza maagizo ya mkuu wa wilaya ya kumaliza kwa wakati madarasa hayo.
Amesema ushirikiano uliopo baina ya madiwani na watendaji katika halmashauri hiyo imekuwa chachu ya kukamilika kwa wakati kwa miradi mingi ya maendeleo na kuwaondolea wananchi kero mbalimbali hivyo kama serikali imeamua kuwasaidia wanaimani mambo mengi mazuri yanakuja katika halmashauri hiyo mpya.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Mhandisi Stephano Kaliwa amesema mpaka sasa wameshapokea fedha hizo na zimeelekezwa katika shule husika na kuahidi kuwa kuanzia sasa ujenzi utaanza mara moja na hakuna atakaekwamisha ujenzi huo.
Wilaya ya Kilombero imepokea zaidi ya shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 133 vya madarasa ya sekondari,madarasa 22 ya shule shikizi,bweni moja la wanafunzi na nyumba moja ya mtumishi katika halmashauri mbili za Mlimba na mji Ifakara.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa