Watu watatu wamejeruhiwa baada ya kung'atwa na mamba katika kijiji cha Nyamwezi kata ya Kiberege katika halmashauri ya wilaya ya Kilombero.
Afisa mtendaji wa kijiji cha Nyamwezi Bi. Neema Lyungu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo lilitokea siku ya pasaka jumapili ya tarehe 16/04/2017 ambapo watu hao watatu walikuwa katika shughuli zao za kawaida za kilimo kandokando ya mto lihegama.
Majeruhi hao wametambulika kwa majina ya Maheli, Kalinganila na bwana Maneno ambapo Maneno alijeruhiwa mguu na kufikishwa katika hospitali ya St francis Ifakara na kupatiwa matibabu kwa kuwekewa vyuma katika mguu, aidha bwana Maheli ambaye ni mkazi wa Kidatu naye alijeruhiwa kisigino cha mguu, wakati bwana Kalinganila amepata majeraha ya mkono.
Mamba hao wanasadikika wametokea katika mto Msolwa ambao kwa kipindi hiki cha masika mto huo humwagwa maji yake katika mto lihegama na kusababisha mamba kuonekana katika maeneo yanayozunguka mto lihegama na maeneo yanayopakana na mto lihegama.
Afisa mhifadhi wanyamapori wa tarafa ya Mang'ula Bwana Haji Ngahungura ameelezea jitihada zilizofanyika ili kuondoa hofu kwa wananchi ni pamoja na kumtafuta mamba huyo kwa kutumia siraha ya bunduki jambo ambalo lilishindikana kutokana na mto kuwa na maji mengi hivyo kupelekea zoezi hilo kuwa gumu.
Aidha Bwana Haji (Afisa wanyamapori) kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa kitongoji pamoja na wananchi wa kitongoji cha Ishililo waliendelea na jitihada za kumnasa mamba huyo kwa kutumia mtego wa ndoano za nondo wenye chambo cha mmbwa na kondoo, hata hivyo jaribio hilo halikufanikiwa baada ya mamba huyo kujinasua kwenye mtego huo kwa kunyoosha nondo na kufanikiwa kutokomea.
Wanakijiji wanaozunguka maeneo hayo wametahadharishwa kutoendelea kufanya shughuli zao katika maeneo yanayozunguka mto Lihegama kwa kipindi hiki ambapo jitihada zinaendelea za kumtafuta mamba huyo mpaka pale maji yatakapopungua katika maeneo hayo hatarishi.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa