Pichani juu: baadhi ya wananchi wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya kilombero ndugu James Ihunyo, katika kikao cha maridhiano juu ya uwekaji wa mipaka katika vijiji vilivyopo jirani na pori tengefu wilayani humo.
Mkuu Wa Wilaya ya Kilombero kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na Usalama ya Wilaya na viongozi Wa vyama vya siasa, wamemaliza mgomo uliokuwepo baina ya wananchi na wataalamu Wa wizara za Ardhi na Maliasili, kuhusu uwekaji upya wa mipaka katika vijiji 23 vilivyopo Jirani na pori tengefu wilayani humo.
Hivi karibu wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya makazi, kwa kushirikiana na wizara ya Maliasili na Utalii, waliamua kupitia na kuweka upya mipaka na hatimae kutengeneza ramani za vijiji, zinazotenganisha vijiji na eneo la pori tengefu la Kilombero katika Wilaya tatu za Kilombero,Ulanga na Malinyi.
Mpaka sasa, zoezi hilo limekwisha kamilika katika Wilaya Mbili za Ulanga na Malinyi, na lilitakiwa kuendelea katika Wilaya ya Kilombero lakini zoezi lilikwama baada ya wananchi kuligomea, kwa madai kuwa zoezi hilo halikuwa shirikishi na wataalamu walikuwa na lengo la kumega maeneo yao na hatimae wao kukosa maeneo ya makazi na shughuli za Kilimo.
Na baada ya msuguano huo ndipo timu ya kamati ya ulinzi na Usalama kwa kushirikisha viongozi Wa vyama vya siasa na wataalamu Wa wizara hizo Mbili waliamua kukutana na viongozi Wa kuanzia ngazi ya tarafa hadi vitongoji katika vijiji hivyo 23 ili kuzungumza nao na hatimae kufikia muafaka ili kufanikisha zoezi hilo.
Katika vikao vilivyofanyika katika tarafa Mbili za Mngeta na Mlimba viongozi hao walitoa kero zao na wataalamu kuwaelezea faida ya zoezi hilo hatimae muafaka ulipatikana na zoezi kuanza hivi karibuni.
Muafaka uliopatikana ni kwamba wataalamu hao watafika katika kila kijiji na kufanya mkutano na wananchi ili kuwaeleza faida ya zoezi na baadae kijiji kuteua watu 15 ambao watashirikiana na wataalamu hao kubaini mipaka ya kijiji na hatimae mipaka halali ikibainika itawekwa mipaka na hatimae kutengeneza ramani mpya.
Baada ya kuwekwa mipaka ambayo itakubaliwa na pande zote kitakachofuata ni wananchi kuheshimu mipaka hiyo na ni marufuku kwa wananchi kufanya shughuli za kibinadamu katika eneo LA pori tengefu.
Vijiji vilivyopo wilayani Kilombero ambavyo vitapitiwa na zoezi la kurekebisha mipaka yake ni Lumemo,Mahutanga,Miwangani,Namwawala,Idandu,Kalenga,Ikwambi,Mofu,Miomboni,Nakaguru na Ijia.
Vijiji vingine ni Isago,Luvilikila,Mkangawalo,Chita,Merera,Msita,Chisano,Kalangakelu,Msolwa,Mwembeni,Ipugusa na Ngalimila.
Hata hivyo habari njema ni kwamba kutokana na eneo kubwa la pori tengefu kuvamiwa na wananchi kuendeleza shughuli za kibinadamu serikali imeona ipunguze eneo hilo kutoka ukubwa Wa kilomita za mraba 6500 hadi kufikia kilomita 2900.
Mkuu Wa Wilaya ya Kilombero James Ihunyo amewataka wananchi kuwapa ushirikiano wataalamu hao ili zoezi likamilike kwa wakati na alama zikishawekwa wananchi waelewe maeneo yao halali ili kujiandaa na msimu mpya Wa Kilimo.
Ikumbukwe kuwa eneo la pori tengefu la Kilombero, ndio Chanzo cha uzalishaji Mkubwa Wa Maji katika Mto Kilombero, ambayo ndio tegemeo la uzalishaji Mkubwa Wa umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji, na pia katika eneo la pori tengefu ndipo lipo eneo la Ardhi chepechepe (Ramsar).
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa