Tarehe 28.06.2024 Mkuu wa Mkoa wa Morogoro mhe. Adam Kighoma Malima aliongoza kikao cha tatu cha maandalizi ya maonesho ya nane nane Kanda ya Mashariki mwa Tanzania huko kwenye uwanja wa Mwalimu Nyerere Morogoro Mjini.
Katika kikao hicho, RC Malima amezitaka Halmashauri zote kuzingatia haki za mifugo kwa kuhakikisha wanaandaa mazingira mazuri ya kuhifadhia mifugo pindi wafikapo kwenye uwanja wa maonesho sambamba na kuhakikisha wanaletwa mapema kabla ya maonesho kuanza ili wapate muda wa kupumzika.
Pia, RC Malima ameziagiza Halmashauri zote kuhakikisha zinakamilisha miundombinu ya mifugo, vipando na mabanda ya maonesho ifikapo Julai 19, na Julai 30 kila mkoa uwasilishe kwa kamati ya maandalizi orodha ya zamu za viongozi watakao wakilisha mikoa yao katika siku zote nane za maonesho.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa, amesema lengo kubwa la maonesho ya nanenane ni watu kuja kujifunza na sio Halmashauri kuibuka washindi.
amezitaka Halmashauri zote kwenye maeneo yao ya maonesho kuwe na hodhi kwa ajili ya kuhifadhia maji ili kuhakikisha mazao na mifugo wanapata maji ya kutosha.
Naye Katibu Tawala wa mkoa wa Dar-Es-Salaam Dkt. Toba Nguvila, amezitaka Halmashauri zote 34 kutoka kwenye mikoa minne inayounda Kanda ya Mashariki (Morogoro, Tanga, Pwani na Dar-Es-Salaam) kuhakikisha zinaleta kwenye maonesho mifugo iliyo bora na sio bora mifugo.
Aidha, maadhimisho ya nanenane mwaka huu kitaifa yatafanyika jijini Dodoma, yakiwa na kauli mbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.”
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa