Pichani juu: baadhi ya wananchi na wakazi wa Chita - Merela, wakipita kwenye daraja hilo la miti ambalo ni hatari kwa maisha yao
Mkuu wa mkoa wa Morogoro Mhe. Kebwe Steven Kebwe, jana amekutana na wakaazi wa Chita-Merela na kuwatoa hofu juu ya ujenzi wa adaraja korofi linalounganisha wakaazi wa eneo hilo na mahali pengine.
Akizungumza na wakaazi hao alipofanya ziara kulitembelea daraja hilo, mheshimiwa Kebwe alisema kuwa daraja hilo ni muhimu sana na ni kiungo ambacho kinaunganisha wafanyabiashara wakubwa sana, kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu, hivyo kuwa katika hali kama hiyo iliyopo haitaleta maana kabisa katika kukuza uchumi wa kilombero na nchi ya Tanzania kwa ujumla.
Aidha mheshimiwa kebwe amesema kuwa, kwa asilimia kubwa ya uzalishaji wa mazao ya mpunga hutokea maeneo ya huko, hivyo ni vyema, eneo hilo likashughulikiwa haraka iwezekanavyo ili kurudisha nguvu ya uzalishaji mali kwa wananchi wa eneo hilo.
Akitoa agizo kwa wakandarasi waliopewa shughuli ya kuhakikisha kuwa eneo hilo pamoja na barabara zote zinazounganisha viunga hivyo zinashughulikiwa mapema, mheshimiwa Kebwe amesema kuwa, mkandarasi wa wilaya, mkandarasi mshauri na yule wa TANROAD washirikiane kwenye masuala ya uchanganyaji wa udongo ili kuweza kupata udongo wenye tija utakaowezesha barabara kuwa imara, aidha aliwataka, wafanye kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa daraja hilo linakwisha mapema iwezekanavyo, huku akitoa maagizo kwa mkurugenzi na mkuu wa wilaya ya kilombero kusimamia kazi hiyo na kuwaahidi wananchi kuwa daraja hilo litakwisha mapema kabisa.
Nae mkuu wa wilaya wilaya ya Kilombero ndugu James Ihunyo alisema kuwa, amepokea maagizo ya kusimamia kazi hiyo, huku akiwaomba wananchi kuhakikisha wanaitunza barabara hiyo pamoja n adaraja hilo kwa kutopitisha Ng’ombe mara kwa mara, kwani wanyama hao huharibu sana miundo mbinu ya barabara.
Katika kuhakikisha masuala ya kimaendeleo yanakwenda sawasawa, iliitishwa harambee ya ujenzi wa majengo kadha katika kuleta maendeleo katika eneo hilo, ambapo zaidi ya shilingi milioni 6.7 zilipatikana kutoka kwa wananchi mbalimbali na mifuko ya simenti ipatayo 55 ilipatikana.
Katika kuonyesha kuwa wanajali maendeleo ya eneo lao, wananchi hao walimshukuru sana mkuu wa mkoa, kwa kuwatembelea na kujali matatizo yao, na kuahidi kuwa watatunza miundo mbinu yote itakayojengwa na serikali, na ikiwa mmoja wao atakwenda kinyume na makubaliano hayo, basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa