Mwenyekiti wa Taasisi ya Tulia Trust Fund, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Spika wa Bunge la Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani mhe. Dkt. Tulia Akson, leo tarehe 26.07.2024 amekabidhi nyumba kwa mwananchi wa kijiji cha Chin’ganda Kata ya Chita, aliyekuwa akiishi kwenye mazingira hatarishi yeye pamoja na familia yake.
Wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara, kabla kukabidhi nyumba hiyo, mhe. Tulia amesema Taasisi yake inatoa misaada ya namna hiyo ili kuwapa hamasa watanzania wenye uwezo waone umuhimu wa kuwasaidia watu ambao hakika wanayo mahitaji.
“Sisi tumeamua kutoa msaada kwa kuongea sio kimya kimya ili watanzania wenzetu ambao Mungu amewajalia uwezo, wahamasike na wao kutoa misaada kwa wahitaji walio katika maeneo yao na hata nje ya maeneo yao” alieleza Dkt. Tulia.
Pia, Dkt. Tulia alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi mambo mazuri ambayo Rais Samia ameyafanya katika Halmashauri ya Mlimba, ikiwemo kuridhia ujenzi wa barabara ya lami toka Lumemo Ifakara hadi Chita JKT Mlimba, upatikanaji wa huduma za maji na umeme na ujenzi wa shule, vituo vya afya na Hospitali ya Wilaya.
Hata hivyo, Dkt. Tulia amepokea kilio cha wananchi wa Chin’ganda, ambacho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mlimba mhe. Innocent Mwangasa na Mbunge wa jimbo la Mlimba mhe. Godwin Kunambi amekiwasilisha kwake kumsihi Rais Samia ujenzi wa barabara hiyo ya Lumemo- Chita uanze.
Naye mwananchi aliyejengewa nyumba, amemshukuru sana Dkt. Tulia kwa moyo wake wa upendo na amemuombea baraka katika utekelezaji wa majukumu yake na maisha yake kwa ujumla.
Kwa mujibu wa msemaji wa Tulia Trust Fund, nyumba hii iliyojengwa Chin’ganda ni ya 14 ambapo nyumba zingine zimejengwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo mkoa wa Mbeya.
Aidha, ujio huu wa Dkt. Tulia umekuwa neema kwa mtoto mwenye mahitaji maalumu na Jeshi la polisi Wilaya ya Kilombero kwa sababu ametoa msaada wa kiti mwendo kwa mtoto huyo na boksi 45 za vigae (Tiles) kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la Ofisi ya polisi kwenye kijiji cha Chin’ganda.
MWISHO
Mngeta Kijiji cha Itongoa
Anuani: P.O.BOX 263
Simu: 023 293 1523
Mobile: 0232931523
Barua pepe: ded@kilomberodc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.Haki zote zimehifadhiwa